Friday, April 5, 2019

NYUMBA 20 ZA POLISI ZAJENGWA PWANI.

 Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo akijadiliana jambo na kamanda wa polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)  Wankyo Nyigesa.
............................


NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

ASKARI wa jeshi la polisi mkoani Pwani, wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa makazi ya kuishi, hali inayosababisha kushindwa kuwahi wakati wakihitajika haraka katika dharula za majukumu yao ya kikazi.


Kutokana na hali hiyo, kwasasa jeshi hilo linajenga nyumba 20 za makazi ya askari polisi hao, zitakazogharimu milioni 500 ili kukabiliana na hali hiyo.


Akizungumza wakati alipotembelea ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa Kibaha Mjini, Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alitaka ujenzi huo ,ukamilike ifikapo June 30 mwaka huu, kama Amiri jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ,Dkt. John Magufuli alivyoelekeza.


Alisema ,askari wanapaswa kulinda mali za wananchi na kulinda usalama wa raia hivyo wanatakiwa waishi kwenye mazingira yaliyo bora.


“Kanda maalum ya kipolisi Rufiji imepatiwa milioni 500, pamoja na jeshi la polisi Pwani milioni 500, jumla ni Bilioni moja, ambazo zimetolewa na serikali kuhakikisha askari wanajengewa makazi ya kuishi “


“Hivyo ni wajibu wa jamii, wenye viwanda kushirikiana na serikali na jeshi la polisi kujenga mazingira bora ya askari hawa waweze kutulinda kwa moyo na upendo “alifafanua Ndikilo.

  
Awali akitoa taarifa fupi kwa mkuu wa mkoa huyo juu ya ujenzi unavyoendelea, Kamanda wa polisi Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, alibainisha, kutokana na ufinyu wa bajeti wamepewa milioni 500 na kwa wastani kila nyumba itagharimu milioni 25 mpaka kukamilika kwake.


Aliwashukuru wadau waliojitokeza kusaidia akiwemo Said Salim Bakhresa, jeshi la wananchi wa Tanzania kupitia kikosi cha usafirishaji (KJ 95) ambao waliwapatia lowbed kwa ajili ya kubeba buldoza kutoka bakhresa sugar company huko Bagamoyo.


Wengine ni Chila mkurugenzi wa Creative Intertraders ltd ambae ametoa mifuko 100 ya saruji na Twyford Ceramics (KEDA )ya Chalinze na wengine ambapo amewashukuru na kuomba wadau wengine waendelee kuwashika mkono.


Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa ambayo , Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Magufuli akiwa anazindua nyumba za askari polisi mkoani Arusha ,april 7 mwaka 2018, alitoa maelekezo kwa mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) kwamba atatoa fedha kwa ajili ya makazi ya askari ,ambapo mkoa huo umeanza utekelezaji baada ya kupokea fungu hilo.
 
Kamanda wa polisi Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, akimuonyesha Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, hali ya ujenzi inavyoendelea.
 
 Muonekano wa kazi ya ujenzi wa nyumba 20 za makazi ya askari polisi unavyoendelea Kibaha Mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment