Tuesday, April 30, 2019

MGOMBEA UDIWANI LINDI (CUF) ALALAMIKIA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) BI Rukia Mbasha akimkabidhi ilani ya chama hicho Diwani mteule wa kata ya Mvuleni Mnuli Saidi Khatibu Baada ya kutangazwa na Msimamizi kuwa Amepita kuwa diwani wa kata hiyo Bila kupingwa

 

Diwani Mteule wa kata ya Mvuleni Mnuli Khatibu (CCM) akionyesha ilani ya Chama hicho baada ya kukabidhiwa

 .................................

Na Hadija Hassan, Lindi.


MGOMBEA Udiwani Kata ya Mvuleni, Halmashauri ya Lindi, Mkoani hapa, Chuma Abdurahamani Saidi (CUF) amesikitishwa na maamuzi yaliyofanywa na wasimamizi wa uchaguzi mdogo Wilayani Hapa kumpitisha mpinzani wake, Mnuli Said Khatibu {CCM} Kuwa Diwani wa kata hiyo kwa madai ya  kushindwa kujibu pingamizi zake.


Chuma ametoa masikitisho hayo wakati alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa Habari hiziz, kuhusu kutupiliwa mbali kwa pingamizi lenye vipengele vinne alizokuwa amemuwekea mpinzani wake Mnuli Said Khatibu wa Chama Cha Mapinduzi  {CCM}.


Chuma alivitaja vipengele hivyo kuwa  ni pamoja na mgombea wa {CCM} uhalali wa uraia wake, Kudanganya mwaka aliozaliwa, Majina ya waliomdhamini sio walioweka saini zao kwenye Fomu na tamko la kisheria la mgombea kutosainiwa na Hakimu wa Wilaya, Mkoa, Kamishina au Wakili aliyepata Kibali au kutambuliwa na Serikali.


Kwa upande wa Mnuli mgombea wa {CCM} alimuwekea mpinzani wake Chuma wa {CUF} pingamizi linalohusu kutotoa tamko la kisheria mbele ya Hakimu kama ilivyoelekezwa na kifungu cha 42 {4} {a} cha Sheria ya ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa Namba 4/1979.


Pia, msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata hiyo ya Mvuleni, Ahmed Ally Mpira, amemuwekea pingamizi mgombea wa {CUF} kutowasilisha Picha {4} za rangi za ukubwa na zile zinazotumika kwenye Pasi za kusafiria {Pasport size} zenye muonekano wa rangi nyeupe kwa nyuma kama inavyoelekezwa na Kifungu cha 25 {3} cha kanuni za uchaguzi wa Madiwani {2015}.


Hata hivyo Chuma alisema mpinzani wake Mnuli wa {CCM}, alidai ameshindwa kujibu pingamizi alizomuwekea, ikiwemo kutoonyesha vielelezo kama vile Cheti cha kuzaliwa au cha uraia vinavyomtambulisha ni raia halali wa Tanzania na vitambulisho vya uraia au kupigia kura kwa watu waliomdhamini.


Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa Habari, Msimamizi wa uchaguzi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Samweli  Gunzar, alimtangaza Mnuli Said Khatibu {CCM} kuwa amepita bila kupingwa,baada ya pingamizi aliyomuwekea Mpinzani wake Chuma Abdurahamani Said wa {CUF} kupita.


Gunza akitumia matakwa ya kifungu cha 45 {2} cha Sheria ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa namba 4 ya mwaka 1979, {sura 292} na kwa Mamlaka aliyopewa na Sheria tajwa hapo juu, “Mimi Samweli Warioba Gunzar msimamizi wa uchaguzi Halmashauri yaWilaya ya Lindi Namtangaza mgombea wa (CCM) Mnuli Said Khatibu kuwa amepita bila kupingwa”Alisema Gunzar.


Akitolea ufafanuzi juu ya namna pingamizi za pande  zote mbili zilivyoshugulikiwa Gunzar alidai kuwa pingamizi zote zilishugulikiwa kwa kuzingatia Sheria na kanuni za uchaguzi wa Madiwani , 2015 ambapo msimamizi wa uchaguzi alifanya maamuzi kwa kuzingatia sheria hizo


Hata hivyo alisema baada ya maamuzi hayo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi aliwataarifu Wagombea  wote juu ya maamuzi yaliyofikiwa kwa kuzingatia kanuni ya 27 (1) ya kanuni za uchaguzi wa madiwani ya mwaka 2015 ambapo msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi alitoa nafasi kwa wahusika waliotajwa katika kanuni hiyo ambae hakuridhika na maamuzi kukata rufaa kwa Msimamizi wa Uchaguzi


Kwa upande wake Diwani Mteule wa kata hiyo ya Mvuleni Mnuli Khatibu wa Chama cha Mapinfuzi {CCM} alisema amefarijika na kupita kwa Pingamizi alilokuwa amemuwekea mpinzani wake na kwamba anachosubiri ni kuapishwa ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.


Halmashauri ya Wilaya ya Lindi ni miongoni mwa Halmashauri yenye Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Mvuleni kufuatia kifo cha aliekuwa Diwani wa kata hiyo kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) MHE, IDAROUS YUSUF MANZI


No comments:

Post a Comment