Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS) kwa kushirikina na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi
jijini Dar es Salaam wamepanda miti kando kando ya mto Tegeta.
Katika zoezi hilo lililofanyika
asubuhi ya leo Aprili 05, 2019, Katibu wa chuo hicho Kanali Furahisha Ntahena aliwaongoza
wanafunzi hao wanajeshi kupanda miti.
Kanali Ntahena amesema wamefikia
uamuzi huo kwa lengo la kukabiliana na athari za mazingira ambazo zimeanza
kuonekana kutokana na uharibifu uliofanyika.
Alisema jeshi limeona ipo haja ya
kushiriki kwenye kampeni ya upandaji miti kwa kuwa athari za mazingira
zinapotokea zinaikumba jamii nzima.
“ Athari za mazingira zikitokea
hazichagui, sasa kutokana na uharibifu ambao wote tumeuona tuna kila sababu ya
kushiriki kwenye kampeni hii ya upandaji miti,”
“Tunapanda kando kando ya mto Tegeta
lakini hatuishii hapa tutapanda pia kwenye maeneo yetu na vilevile tutawapa
miti mingine wanajeshi wakapande kwenye makazi yao,” Alisema Kanali Ntahena.
Katika zoezi hilo jumla ya miti 2,000
ilipandwa kwenye mto huo ambao umeathiriwa na shughuli za kibinadamu.
Kwa upande wake Meneja wa TFS wilaya
ya Kinondoni Dotto Ndumbikwa ameziomba taasisi na watu binafsi kushiriki kwenye
kampeni ya upandaji miti ili kutunza mazingira.
“Ikitokea la kutoa kutokana na athari
za uharibifu wa mazingira tutakaoathirika ni wote, hivyo ni muhimu kila mmoja
kwenye nafasi yake akatunza mazingira,”
Ndumbikwa ameeleza kuwa katika wilaya
yake ya Kinondoni uharibifu wa mazingira ni mkubwa na unachangiwa na shughuli
za kibinadamu ikiwemo uvamizi katika maeneo ya mito.
No comments:
Post a Comment