Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasha Mwenge kuashiria kuzinduliwa kwa
mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Mlowo mkoani Songwe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge
Kitaifa kwa mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi kuashiria
kuanza kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019.
Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
....................................
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Wananchi wote wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutumia mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019
kumkumbuka Baba wa Taifa kwa kupinga vitendo vya dhulma, ufisadi, rushwa,
maradhi, chuki, dharau na kuwataka kuenzi umoja na mshikamano wetu kuchapakazi
kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo
kwenye sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa zilizofanyika kwenye
uwanja wa Mlowo mkoani Songwe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na
Serikali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa.
Kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru
mwaka 2019 ni “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze
vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
“Nimependezwa na kaulimbiu hii ambayo
inauwiano wa moja kwa moja na jukumu langu la kila siku la kusimamia na kutunza
mazingira ya nchini. Sote tunafahamu kuwa bila utunzaji thabiti wa mazingira
basi vyanzo vya maji hupotea”alisema Makamu wa Rais
Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji
safi na salama nchini inaendelea kuimarika ambapo huduma ya maji
vijijini imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 58.7 kwa
mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 64.8 mwezi februari 2019 na miji mikuu ya
mikoa kutoka asilimia 78 mwezi machi 2018 mpaka asilimia februari 2019.
“Niwahakikishie wananchi
tutatekeleza kwa vitendo ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inayotutaka
kuboresha huduma ya maji vijijini kufikia asilimia 85 na mijini kwa asilimia 95
ifikapo 2020”alisisitiza Makamu wa Rais
Aidha, Makamu wa Rais kupitia hadhara
ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019 ametoa wito kwa
wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kufanya shughuli za
kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, ujenzi, ukataji na uchomaji miti kwenye
vyanzo vya maji.
Makamu wa Rais pia amewakumbusha
wananchi juu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwezi oktoba 2019
kuhakikisha wanachagua Viongozi wachapakazi na wenye dhamira ya maendeleo kwa
jamii.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019
zitaongozwa na Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi
No comments:
Post a Comment