Naibu Waziri Kilimo Omary
Mgumba akiwa pamoja na Mgeni wake Makamu wa Rais wa Kampuni ya OCP Afrika
Mashariki, Bwana Faysal Benameur (Kulia kwake) pamoja na Watendaji wa Kampuni
ya OCP Barani Afrika na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara ya Kilimo mara
baada ya kumalizika kwa Mkutano wao, Jijini Dodoma, jana Aprili 04, 2019.
...................................
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo,
Mhe. Omary Mgumba amewaeleza Wawekezaji kutoka nchini Moroco ambao ni Kampuni
ya Mbolea ya Taifa (OCP) ya nchini kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi za
kuendeleza kilimo na amewahakikishia kuwa Serikali itahakikisha inawasaidia ili
wafanikishe azma yao ya kujenga kiwanda cha mbolea mkoani Lindi katika wilya ya
Kilwa.
Naibu Waziri Mgumba akiwa pamoja na
Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa Mikutano wa
Wizara ya kilimo Jijini Dodoma amemwambia Makamu wa Rais wa Kampuni ya OCP
Afrika Mashariki, Bwana Faysal Benameur mapema leo kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano imedhamiria kumwinua Mkulima wa Tanzania ambapo mkazo umewekwa katika
kuongeza uzalishaji na tija kwenye mazao ya chakula na biashara na kwamba
ujenzi wa Kiwanda cha mbolea nchini utachochea katika ongezeko la uzalishaji na
tija.
Waziri Mgumba amesema nchi zote
zilizoendelea, zimepiga hatua kubwa katika Sekta ya Kilimo kwa kuwa
zinazingatia matumizi makubwa ya mbolea yanaenda sambamba na eneo la uzalishaji
pamoja na kutibu hitaji la mapungufu ya virutubisho vilivyo kwenye udongo na si
ilimradi kutumia mbolea tu.
Naibu Waziri wa Kilimo Mgumba
ameongeza kuwa uwiano wa matumizi ya mbolea na eneo la kilimo hapa nchini upo
chini sana, ukilinganisha na nchi za Afrika na zile zilizoendelea, akitoa mfano
amesema, hapa Tanzania, matumizi ya mbolea ni kilo 20 kwa hekta, Ethiopia na
nchi nyengine za Afrika ni kilo 100 kwa hekta wakati nchini Marekani na nchi
nyingine, zilizoendelea matumizi yao ya mbolea ni kilo 1,000 (Sawa tani 1) kwa
hekta.
“Kwa uwiano huu, hatuwezi kuzalisha
kwa kiwango kikubwa na ndiyo maana tija ipo chini, nitoe mfano, kwenye
uzalishaji wa mahindi, Tanzania tunazalisha tani mbili (2) kwa hekta huku
Ethiopia ikizalisha tani sita (6) kwa hekta wakati Marekani, wanazalisha tani
kumi (10) hadi kumi na mbili (12). Amekaririwa Mhe. Mgumba.
“Napenda Wakulima wa Tanzania wafahamu
kuwa suala la muhimu si kutumia tu mbolea, lazima tujenge mazingira mazuri ya
kufahamu mahitaji halisi ya virutubisho vinavyokosekana kwenye udongo, ardhi
yetu imelimwa na mababu na mababu, na wazazi wetu, na wao wameshafariki,
hatutaweza kuzalisha kwa tija bila kutumia mbolea”. Amesisitiza Naibu Waziri
Mgumba.
“Nawapongeza Kampuni ya OCP kwa
kuliona jambo hilo na huo ndiyo msimamo wao na watatusaidia kwa kuwa wanavifaa
vya kufanya tathmini ya udongo kabla ya kuwauzia Wakulima mbolea.” Amekaririwa
Mhe. Mgumba.
Naye Meneja wa Kampuni ya Mbolea ya
OCP (Tanzania) Dkt. Mshindo Msolla amesema Kampuni hiyo inataraji kujenga Vituo
vya kufanya majaribio ya kuonyesha namna zoezi la upimaji wa udongo
linavyofanyika, matokeo baada ya kupima na matumizi ya mbolea za OCP kulingana
na matokeo ya taarifa hizo na kuongeza kuwa tarehe 8 Aprili wanataraji kuzindua
Kituo kimoja Mkoani Songwe.
Waziri Mgumba amesisitiza kuwa Vituo
(Ward Resources Centre) kama hivyo vinapaswa kujengwa katika ngazi ya Tarafa
ambapo Serikali ilishajenga vituo hivyo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya
Kilimo Awamu ya Kwanza (ASDP I) na kuongeza sasa ni wakati muhafaka wa
kuviendeleza.
Kampuni ya Mbolea ya OCP ipo katika
mazungumzo ya kujenga kiwanda cha mbolea katika mkoa wa Lindi Wilaya ya Kilwa
ambapo jumla ya dola bilioni 1.7 zinataraji kuwekezwa katika mradi huo mkubwa
ambapo kwa kuanzia Kampuni ya OCP imeanza kujenga mashine ya kuchanganya
virutubisho vya madini mbalimbali ili kupata mbolea za iana tofauti hapa nchini.
Imeelezwa kuwa ujenzi wa Kiwanda
hicho cha mbolea utasaidia kupunguza gharama ya bei ya mbolea kwa zaidi ya
asilimia 30 hadi 40.
Naibu Waziri Omary
Mgumba akiwa pamoja Meneja wa Kampuni ya OCP Tanzania, Dkt. Mshindo Msolla
katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya kilimo Jijini Dodoma, jana tarehe
4/4/2019.
Naibu Waziri Omary
Mgumba akiwa pamoja Mgeni wake Makamu wa Rais wa Kampuni ya OCP Afrika
Mashariki, Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara ya Kilimo pamoja na Watendaji wa
Kampuni ya OCP Barani Afrika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya kilimo
Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment