Thursday, April 4, 2019

RIDHIWANI KIKWETE AENDELEA KUTEKELEZA AHADI ZAKE JIMBONI KWAKE.

 MBUNGE wa jimbo la Chalinze,wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani  Kikwete (mwenye kofia ya CCM) akiwa katika jimbo lake kupitia miradi mbalimbali ambayo aliitolea ahadi wakati wa kuomba kura mwaka 2015.
..................................................

Na  Shushu  Joel,Chalinze. 

MBUNGE wa jimbo la Chalinze,wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani  Kikwete ameendelea na  ukamilishaji wa ahadi zake alizokuwa amewaahidi wananchi  wa jimbo lake pindi alipokuwa akijinadi kuwaomba kura ili aweze kuwasaidia kuwasemea bungeni  ili serikali  itatue  changamoto  zao kwa wakati.

Maneno  hayo alisema jana katika kijiji cha chahua kata ya Bwilingu jimboni humo alipokuwwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.

Akizungumza  na wananchi wa eneo hilo  mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingI Kikwete amewapongeza  wananchi hao kwa usimamizi mzuri wa fedha alizochangia katika ujenzi huo uliogharimu zaidi ya milioni 40 mpaka sasa.

"Uwepo wa zahanati katika kijiji hiki  utapunguza kama si  kuondoa  kabisa vifo vya  wazazi na watoto ambavyo sio  vya lazima"Alisema Kikwete.

Aliongeza  kuwa  wakati anawaomba wananchi hao ridhaa ya kuwa kiongozi wao aliwahakikishia kabla ya miaka 5 kumalizika atahakikisha anajenga zahanati katika kijiji hicho na hivyo jambo hilo limekamilika kwa asilimia 90.

Aidha  amewataka wananchi hao pindi zahanati hiyo  itakapoanza kufanya kazi wapendelee kupima afya zao ili kuweza kubainika nini  kinachowasumbua ili wataalamu waweze kubaini  tatizo  na kutatuliwa.

Aidha, mbunge  huyo  amewahakikishia wananchi wa jimbo hilo kuwa kila  alichokiahidi atatekeleza kabla ya miaka 5 kumalizika cha msingi  katika miradI yote inayoletwa na serikali kwa ushawishi  na ile mingine  inapaswa kulindwa ili itumike  kwa vizazi  vingi.

Kwa upande wake Fatuma Ally mkazi  wa eneo hilo amempongeza mbunge huyo, kwa jinsi anavyopambana kwaajili ya wananchi wa kijiji hicho katika kuhakikisha wanapata maendeleo ya kila nyanja ili kuondokana  na changamoto za hapa na pale.

Aliongeza kuwa mbali na uwekaji wa jiwe la msingi katika zahanati hiyo pia umetuletea umeme, kisima kikubwa cha maji na utengenezaji wa miundombinu inayosaidia kurahisisha kwa shughuli za ufanisi wa maendeleo katika maeneo yetu.

Aidha  amempongeza Kikwete kwa jinsi alivyofanikisha ujenzi wa shule  ya msingi iliyokuwa imechakaa kwa ujenzi wa madarasa  matatu hivyo hali hiyo  imessaidia kuchochea kwa mahudhurio mazuri ya watoto shuleni na kupata masomo yao ya kila siku.

Naye Abeid Salmu ambaye ni shehe  wa msikiti wa kijiji hicho amempongeza Kikwete kwa juhudi zake za ufanisi wa kuwaletea  maendeleo mbali mbali kwenye kijiji hicho bila kuchelewesha.

"Kijana  wetu  Ridhiwani amekuwa akijituma sana katika uletaji wa maendeleo hivyo tunamuomba  aendelee utekelezaji huo huo kwa wananchi wake"Alisema.

Aidha shehe huyo amemtoa wasiwasi mbunge huyo kuwa katika jimbo la Chalinze hakuna mbunge mwenye moyo kama wake hivyo asijitokeze mtu yeyote  yule kuleta uso  wake katika uchaguzi ujao kwani sie tunamjua Kikwete ndio kimbilio letu  kwani muda  mchache tu kafanikisha miradI mingi  na mikubwa Chalinze.
 
MBUNGE wa jimbo la Chalinze,wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani  Kikwete (mwenye kofia ya CCM) akiwa katika jimbo lake kupitia miradi mbalimbali ambayo aliitolea ahadi wakati wa kuomba kura mwaka 2015.
 

No comments:

Post a Comment