Thursday, April 11, 2019

WATOTO 58,048 KUPEWA TIBA KINGA CHALINZE

Image may contain: 3 people, people standing and indoor
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo Bi Amina Kiwanuka amezindua rasmi zoezi la utoaji tiba kinga ya kichocho na minyoo tumbo kwa watoto 58,048 wenye miaka 5-14 walioandikishwa shule na wasioandikishwa,uzinduzi huo umefanyika leo katika shule ya msingi Lugoba kiwilaya.


Katika hotuba yake ya uzinduzi wa zoezi la utoaji tiba kinga ya kichocho na minyoo tumbo,Mkurugenzi Kiwanuka amewaasa wanafunzi na walimu kuwa walimu kwa jamii kwa kutoa Elimu ya matumizi ya maji safi na salama ili kujiepusha na kichocho na minyoo tumbo na kuwataka wanafunzi waache kuoga kwenye madimbwi ya Maji ambayo kimsingi huwa ndio chanzo cha Magonjwa kama kichocho.

 
Kwa mujibu wa Mratibu Wa Magonjwa yaliyokuwa hayakupewi kipaumbele, Dkt Waziri Mkuwili alifafanua kuwa zoezi hili linafanyika siku ya leo katika shule zote katika Halmashauri ya Chalinze kwa kuwapa tiba kinga ya kichocho na minyoo tumbo jumla ya watoto 58,048 wenye umri wa miaka 5-14 katika halmashauri ya Chalinze.


Aliendelea kufafanua kuwa zoezi hili ni zoezi la kitaifa ambalo linafanyika kitaifa kwa misingi ya kupambana na Magonjwa ambayo hayakupewa kipaumbele na hatimaye kuathiri Afya za watoto katika jamii.


Hata hivyo Dkt Mkuwili alifafanua kuhusu ubora wa dawa hizo na kuwataka wananchi wasisite kuwaleta watoto wao katika vituo vya kutolea dawa na kuongezea kuwa dawa hizi hazina madhara kwa watoto kinachotakiwa ni kuhakikisha watoto wamekula chakula ndiyo waweze kumeza dawa hizo.


Naye Mganga Mkuu Wa Wilaya Dkt Rahim Hangai aliwataka wananchi wa Chalinze kuwaleta watoto katika vituo vya dawa kwani leo ni siku rasmi kwa ajili ya zoezi la kunywesha dawa watoto wote katika Halmashauri ya Chalinze wenye umri wa miaka 5-14

No comments:

Post a Comment