Rais Dkt John Pombe Magufuli
amewahakikishia wananchi wa Nanyamba, Tandahimba, na Newala Mkoani Mtwara
kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya uhakika ili kuunganisha
Kanda ya Kusini Kiuchumi na wananchi wa Mkoa huo kuendelea kufanya kazi kwa juhudi
ili kuweza kujiletea maendeleo yao.
Akizungumza katika maeneo mbalimbali
ya Mkoa huo, Rais Magufuli amesema Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya
Mtwara-Tandahimba-Nanyamba yenye urefu wa kilometa 50 itakayogharimu kiasi cha
Tsh.bilioni 86 na kumwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack
Kamwelwe kutangaza zabuni ya ujenzi wa kilometa zingine na kufikia kilometa 100
na hivyo kuunganisha kwa urahisi nyanda za kiuchumi katika mikoa ya kusini.
“Barabara hii itakuwa ni kiunganishi
cha uchumi mikoa ya kusini, hatuwezi kushindwa kujenga kilometa 100, lengo letu
kuu ni kuiunganisha Bandari yetu ya Mtwara na mizigo inayotoa Malawi,” alisema
Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema kuwa
katika kuwainua wakulima wa Mkoa wa Mtwara, ambapo Serikali imetekeleza ununuzi
wa korosho kutoka kwa wananchi wenye korosho zaidi ya kilo 1500, na Tsh Bilioni
50 tayari zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao, na kwa upande wa
wakulima wa korosho wenye kilo chini ya 1500 wamelipwa kiasi cha Tsh Bilioni
578.
Rais Magufuli amewahiza
wafanyabiashara walanguzi wa zao la korosho ‘Kagomba’ kuacha kuwadhulumu
wakulima wadogo kwa kuwapa bei ambayo hailidhishi huku wakijua wametumia
gharama kubwa katika kuendeleza zao hilo, na kusema serikali ya Awamu ya tano
haitarudi nyuma kuwatetea wakulima hao.
“Utakuta mtu amelima korosho zake,
amenunua madawa, ametumia gharama kuzivuna unakuja kumpa bei ya 1500, kwa
Serikali ya Awamu ya Tano hili halikubaliki”, alisema Rais Magufuli.
Akiongelea miradi mingine
inayotekelezwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni pamoja na upanuzi wa
bandari ya Mtwara, , upanuzi wa uwanja wa Ndege na ukarabari wa mradi wa maji
wa makonde ambao utagharimu kiasi cha Tsh.bilioni 160 zikiwa ni fedha za mikopo
kutoka Serikali ya India unaowezesha ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28
nchini.
No comments:
Post a Comment