Tuesday, April 16, 2019

DC BAGAMOYO AGAWA SUKARI YA MAGENDO KWA TAASISI ZENYE UHITAJI.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo  Bi Zainabu Kawawa, akimkabidhi Mkuu wa Gereza la Kigongoni, Mrakibu wa Magereza SP-Muyengi Bulilo, aliyesimama kulia ni
Afisa Forodha Mfawidhi kituoa cha forodha bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa.
 
 Afisa Forodha Mfawidhi kituoa cha forodha bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa, akizungumza wakati alipomkabidhi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Sukari iliyoingizwa wilayani humo kwa njia ya Magendo
   Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo  Bi Zainabu Kawawa, (kushoto) akipokea sukari iliyoingizwa kwa njia ya magendo, kutoka kwa Afisa Forodha Mfawidhi kituoa cha forodha bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa.
................................................ 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo  Bi Zainabu Kawawa amegawa sukari mifuko 227 yenye ujazo wa kilo 50 kila mmoja ambayo iliingizwa katika wilaya hiyo kwa njia za magendo.


Akikabidhi sukari hiyo kwa wakuu wa shule na wakuu wa vituo vya kulelea watoto yatima na wanye mazingira magumu, Mkuu huyo wa wilaya amewaonya wafanyabiashara wanaongizi bidhaa zao wilayani humo kupitia bandari bubu.


Alisema Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya wilaya imejipanga vyema kuhakikisha wanadhibiti mianya ya wale wanaokwepa ushuru wa serikali.


Alisema amefanya juhudi ya kusimamia idara zinazohusika kurahisisha masharti ya uingizaji bidhaa katika bandari ya Bagamoyo hivyo wafanyabiashara hawana sababu ya kupitisha bidhaa zao kwa njia za magendo.


Alifafanua kwamba ameitisha kikaona cha wafanyabiashara pamoja na idara za serikali ili kuondoa urasimu wa vibali vya kuingiza bidhaa ikiwa ni njia ya kuwasaidia wafanyabiashara hao wasikwepe ushuru wa serikali.


Alizitaja idara ambazo amezikutanisha na wafanyabiashara hao kuwa ni Mamlaka ya chakula na Dawa nchini (TFDA) Mamlaka ya mapato nchini (TRA) Mamlaka ya Bandari (TPA) Idara ya forodha na ushuru wa bidhaa, pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama lengo lilikuwa ni kutoa maelekezo nafuu yatakayowawezesha kutumia bandari halali ya Bagamoyo ili serikali iingize mapato kupitia bidhaa zinazoingia katika wilaya hiyo.


"Nimewakutanisha wafanyabiashara wote wanaoingiza bidhaa katika wilaya yangu na TFDA, TRA, TPA watu wa idara ya Forodha ili kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara,  hiyo ni kazi yangu na nimeisimamia"
"Sasa sitarajii baada ya hapo bado kuwe na watu wanaokwepa ushuru wa serikali watakuwa na sababu zipi kama sio kukiuka sheria halali ya kulipa kodi na suhuru?" Alihoji mkuu huyo wa wilaya.


Wakati huohuo amewaonya wale wote aliowagawia sukari hiyo kuitumia kwa mujibu wa maelekezo yake na wala wasiitumie kwa manufaa yao binafsi.
Alisema endapo atabaini kuna mtu ametumia sukari hiyo kinyume na utaratibu atamchukulia hatua za kinidhamu.


Awali akitoa taarifa kwa mkuu wa wilaya wakati wa kukabidhi sukari hiyo, Afisa Forodha Mfawidhi kituoa cha forodha bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa, amesema sukari hiyo iliyokamatwa imeingizwa katika wilaya ya Bagamoyo kwa njia za magendo na kwa idhini ya kamishna wa forodha na ushuru wa bidhaa nchini imekabdihiwa kwa mkuu wa wilaya ili agawe kwa taasisi zenye uhitaji.


Alisema uagizaji wa sukari una utaratibu wake hapa nchini hivyo sukari hiyo haikufuata utaratibu na kwamba wameikamata na kuitafisha.


Aliwataka wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa katika bandari ya Bagamoyo kufuata utaratibu uliowekwa kisheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kuwapata.
Aliongeza kwa kusema kuwa, idara ya forodha kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama imejipanga kudhibiti bandari bubu zote wilayani humo.


Alionya kuwa, wananchi wasikubali kuhifadhi sukari ambazo zimeingizwa kinyume na utaratibu na kwamba ikukutwa kwenye nyumba na mwenye nyumba atahusika na magendo hayo.


Alisema wanaomiliki vyombo vya usafiri kama gari, na pikipiki wanapaswa kuwa makini na mizigo wanayobeba kwani gari au pikipiki ikikamatwa na bidhaa ya magendo vyote vinataifishwa na kuwa mali ya serikali.


Nae Afisa forodha Mwandamizi Bandari ya Bagamoyo, Noeli Makere amewataka wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa wilayani humo kuacha kufanya biashara za magendo ili kuepuka hasara wanazopata mara kwa mara.


Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara kuwa wazalendo na nchi yao kwa kulipa kodi stahikibila bila ya shuruti ili kuunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuli katika kukusanya mapato ya serikali.


Amesema kila mwananchi anapaswa kutoa ushirikiano ili kukabiliana na biashara za magendo kwakuwa jukumu la kukabiliana na magendo ni la watanzania wote.


Akizungumza kwa niaba ya wenzie, Mkuu wa shule ya Sekondari Bagamoyo, Khalfani Milongo amesema anaishukuru serikali kwa kugawa sukari kwenye shule kwakuwa bado kuna uhitaji wa bidhaa hiyo.


Alisema watahakikisha wanaitumia sukari hiyo kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa maelekezo ya mkuu wa wilaya.


Nae mlezi wa watoto katika kituo cha kulelea watoto wenye mazingira magumu, cha Kamelot Children Home, Sister Sikaria Sevelin amesema sukari hiyo itawasaidia katika kuwahudumia watoto waliopo ndani na nje ya kituo.


Aidha, ameishukuru serikali kupitia kwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, kwa kutoa ushirikiano katika vituo kama hivyo jambo ambalo linawapa moyo wa kuendelea kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
 

Sukari ya magendo iliyokamatwa Bagamoyo ikipakiwa kwenye gari la magereza ili kupelekwa gerezani.

 

Walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari  Bagamoyo pamoja na wasimamizi vituo vya kulelea watoto yatima na wenye mazingira magumu, wakiwa katika pfisi ya Mkuu wa wilaya Bagamoyo, kwaajili ya kugaiwa sukari iliyokamatwa baada ya kuingizwa kwa njia ya magendo.

 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo  Bi Zainabu Kawawa, (kushoto) akikabidhi sukari kwa wafanyakazi wa kituo cha kulelea watoto wenye mazingira magumu cha Kamelot Children Home kilichopo kitongoji cha Mji mpya kata ya kisutu wilayani humo.

 
 Mlezi wa watoto katika kituo cha kulelea watoto wenye mazingira magumu, cha Kamelot Children Home, Sister Sikaria Sevelin (kulia) akimuonyesha mkuuwa wilaya vyumba wanavyolala watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo  Bi Zainabu Kawawa, akizungumza na watoto wanaolelewa katika kituo cha Kamelot Children Home kilichopo kitongoji cha Mji mpya kata ya kisutu wilayani humo, mara alipotembelea kituoni hapo na kuwagawia sukari. 

No comments:

Post a Comment