Sunday, August 11, 2019

SADC kuanzisha mfuko wa kilimo wa kanda



Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema ipo kwenye mkakati wa kuanzisha mfuko wa kilimo wa kanda kwa ajili ya kusaidia nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Hayo yamesemwa leo Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kilimo, Chakula na Maliasili wa jumuiya hiyo Domingos Gove wakati anazungumza na waandishi wa habari za mikutano ya SADC inayoendelea jijini.

“Kwa sasa tupo katika mkakati wa kuanzisha mfuko wa kilimo wa pamoja wa kikanda ambao lengo ni kuhakikisha tunasaidiana katika chakula kwa nchi za SADC,” amesema Gove.

Amefafanua katika mkakati huo pia watahakikisha kunakuwa na miundombinu itakayofanikisha nchi wanachama zinajikita kwenye kilimo kwa ajili ya kupata chakula cha kutosha kwa nchi zao.

Mkurugenzi huyo wa Kilimo, Chakula na Maliasili ameongeza kuwa kwenye mfuko huo ambao utaanzishwa kwa nchi za SADC utahakikisha kunakuwa na usambazaji wa mbegu bora zisizo na magonjwa, upatikanaji wa soko kwa malighafi zinazohusika kwenye suala la kilimo.

Pia amesema mikakati mingine ni kuongeza ushindani na uzalishaji wa nafaka pamoja na kuhakikisha kunakuwa na sera ya kulinda usalama wa chakula.

No comments:

Post a Comment