Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, zainabu kawawa, akizungumza na wananchi wa kata ya Kiwangwa alipofanya ziara kusikiliza kero za wananchi, katikati ni Katibu tawala wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni.
................................
Mkuu
wa wilaya ya Bagamoyo, zainabu kawawa amewaonya wenyeviti wa vitongoji na
vijiji wilayani humo kuacha tabia ya kuwakaribisha wafugaji wageni ili kuepuka
migogoro ya wafugaji na wakulima wilayani humo.
Mkuu
huyo wa wilaya ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya,
ameyasema hayo katika ziara yake aliyoifanya kwenye vijiji vya kata za Kiwangwa
na Fukayosi iliyolenga kusikiliza kero za wananchi.
Katika
ziara hiyo ambayo alipata nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara na kuwapa
nafasi wananchi kueleza kero zao ambapo wakulima wamelalamikia wafugaji
kuingiza mifugo yao kwenye mashamba yenye mazao hali inayopelekea wakulima
kushindwa kuvuna kile walichopanda.
Wakulima
hao walimueleza Mkuu wa wilaya kuwa, wenyeviti wa vijiji na vitongoji wamekuwa
chanzo cha migogoro hiyo kwakuwa wanawakaribisha wakulima wageni ambao
hawafuati taratibu zilizowekwa katika vijiji hivyo.
Akitoa
majibu mbele ya Mkutano wa hadhara, Mkuu huyo wa wilaya alisema wenyeviti wa
vitongoji wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sheria
ili kuepuka kuleta migogoro kwa wananchi.
Alisema
mwenyekiti yeyote wa kitongoji au kijiji atakaehusika kuwakaribisha wafugaji
wageni atamchukulia hatua za kisheria na kinidhamu kwani kitendo hicho
kinachangia migogoro.
"Kama
umeshindwa kuwahudumia wananchi kwenye kitongoji chako mpaka uchukue chochote
kitu kutoka kwa wafugaji ili uwakaribishe na hali unajua huna eneo kwenye
kitongoji chako, nikianza operesheni yangu ya kuondoa wafugaji wageni nitaanza
na wewe Mwenyekiti wa Kitongoji, Alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Aliongeza
kwa kusema kuwa kitendo hicho ni kuniharibia mazingira yangu ya kazi na kwamba
yeye hayuko tayari kuharibiwa kazi na wenyeviti wa vitongoji au vijiji.
Alisema
wilaya ya Bagamoyo tayari ina wafugaji ambao wamesajiliwa katika vijiji vyao na
kutengewa maeneo kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi hivyo si vyema kuleta
wafugaji wageni ambao hawana maeneo ya kupeleka mifugo yao.
Aidha,
amewaonya pia wafugaji kuacha kuwakaribisha wafugaji wenzao kutoka maeneo
mengine ili kuepuka migogoro ya wafugaji na wakulima ambayo imebainika
inasababishwa na wageni.
Kwa
upande wao wafugaji wamesema watashirikiana na serikali kuwaondoa wafugaji
wageni kwakuwa hata wao wanapata madhara kutoka kwa wafugaji wageni.
Wamesema
kuwepo kwa wafugaji wageni kumekuwa na madhara ya aina nne kwenye maeneo yao
ambayo ni wafugaji wageni huvamia kwenye malisho ya wenyeji na kufanya wenyeji
kukosa sehemu ya kulisha, wizi wa mifugo, kuleta magonjwa ya kuambukiza ya
wanyama na pia wafugaji wageni wamekuwa na tabia ya kubaka mabinti wenyeji wa
maeneo husika.
Kufuatia
hali hiyo, Mkuu wa wilaya amemuagiza Mkuu wa polisi wilaya ya Bagamoyo,
kuchukua maelezo ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Segwa na katibu wake ili
kuwabaini wale walifanya vitendo viovu kwenye eneo hilo na hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yao.
Wenyeviti wa vitongoji kata ya Kiwangwa wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Mkuu wa wilaya.
Baadhi ya wafugaji wakimsikiliza Mkuu wa wilaya katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Kiwangwa.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bagamoyo, wakifuatilia mazungumzo ya Mkuu wa wilaya hiyo alipofanya mkutano wa hadhara kata ya Kiwangwa.
Baadhi ya wananchi wakisikiliza mazungumzo ya Mkuu wa wilaya alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Kiwangwa.
No comments:
Post a Comment