Thursday, August 1, 2019

WATUMISHI KIBAHA WAMKERA MKONGEA

Image may contain: 2 people, crowd and outdoor
Na Omary Mngindo, Mlandizi.

IDADI ndogo ya Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani waliofika katika mradi wa ujenzi wa hospitali wilayani humo, imemkera kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019 Mzee Mkongea Ally.


Tukio hilo limetokea muda mfupi baada ya Mkongea na wakimbiza Mwenge wenzake, walipomaliza kukagua majengo saba ya hospitalini hapo, inayojengwa eneo la Chekeleni ndani ya Kata za Kawawa na Kikongo wilayani hapa.


Kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Assumpter Mshama, Mbunge wa jimbo Humoud Jumaa na viongozi mbalimbali, Mkongea amesikitishwa na uchache wa watumishi hao, huku akisema kitendo hicho kinaonesha dharau mbele ya viongozi wao.


"Idadi ya watumishi waliopo ni ndogo sana, ukilinganisha na waliotupokea asubuhi na hata pale tulipokula, hapa hata ukipiga lokoo utabaini kabisa watumishi ni wachache sana," alisema Mkongea.


Aliongeza kuwa kitendo cha watumishi hao kutowaheshimu viongozi wao ni utovu wa nidhamu, huku akihoji kama angekuja Rais Dkt. John Magufuli wangeweza kufanya jambo kama hilo?


"Viongozi wetu waasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume wamefanyakazi kubwa katika nchi hii, tumuheshimu Rais rais wetu Dkt. John Magufuli kwani ndiye aliyetupatia ajira tuliyonayo, pia tuuheshimu Mwenge wa Uhuru," alisema Mkongea.


Baada ya kauli hiyo, Mkuu wa wilaya Mshama nae alisikitishwa na kitendo cha watumishi hao, na kumweleza kiongozi huyo kwamba watumishi katika halmashairi hiyo wana dharau kubwa, huku akisema kuwa lazima hatua za nidhamu zichukuliwe dhidi yao.


Mshama akawataka watumishi waliopo eneo hilo wasimame kwa mstari wajiorodheshe idadi na majina yao, kwa lengo la kuwabaini wasiokuwepo eneo hilo la Mwenge, huku akiwataka viongozi wa idara kuongoza mstari.


"Watumishi wa halmashauri ya Kibaha wanadharau sana, siku chache kabla ya Mwenge nilikaa nao nikawaeleza kuhisiana na nidhamu, lakini wameshindwa kinielewa," alisema Mshama.

No comments:

Post a Comment