Thursday, August 1, 2019

POLISI PWANI WATOA ELIMU KWA MADEREVA

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA PWANI.

Leo tarehe 01/08/2019. Kumefanyika mafunzo kwa madereva wanaoendesha mabasi ya abiria kupitia Mkoa wa Pwani ambao wamefanya makosa mbalimbali hatarishi kama ifuatavyo:-


1. Kuendesha gari kwa mwendokasi. 2. Matumizi mabaya ya gari barabarani (wrong overtaking). 3. Kuendesha gari wakiwa wametumia kilevi. 4. Kuzidisha abiria kupita kiasi.


Utoaji wa mafunzo haya umekuwa ni mwendelezo wa kuwapatia elimu madereva wafanyao makosa ambapo hadi sasa mafunzo hayo yameshatolewa kwa awamu tano na mafunzo ya leo yakiwa ni ya awamu ya sita na madereva 12 wa mabasi wameweza kushiriki kati ya 27 waliopaswa kuhudhuria darasa hilo la wiki moja.


Utoaji elimu huu unaofanyika ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Taifa la Usalama barabarani kupitia kamati ya usalama barabarani Mkoa wa Pwani ambao walijiwekea mkakati wa kukabiliana na ajali katika maeno matatu ambayo ni:-


a) Kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara na hili limekuwa likifanyika katika vituo vya mabasi na vijiwe vya bodaboda kwa kushirikiana na mabalozi wa usalama barabarani kundi la maigizo la Mizengwe.


2. Kufanya Oparesheni- katika hili madereva mbalimbali wameweza kukamatwa na miongoni mwao ndio hawa wanaopatiwa elimu sasa.


3. Kusimamia sheria- askari wamekuwa wakipangwa katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanasimamia sheria ipasavyo na kwa wale wanaokiuka kuadhibiwa kwa tozo la papo kwa papo.


Aidha, darasa hilo liliwajumuisha madereva 11 wa Polisi kutoka Wilaya zote lengo likiwa ni kuwakumbusha sheria za usalama barabarani na kuwajengea umahiri kwa vyombo vya serikali wanavyovitumia kila siku.


Kadhalika, elimu hii imetolewa kwa ushirikiano na wadau wengi waliowasilisha mada zao kutoa Chuo cha VETA- Kipawa, askari kutoka kitengo cha elimu Mkoa wa Pwani, Wakaguzi wa magari, wajumbe wa kamati ya usalama barabarani Mkoa wa Pwani toka Taasisi za Serikali- VETA Pwani, LATRA na Jeshi la Zimamoto.


Madereva wote wameweza kufundishwa yafuatayo:- i) Sheria, Kanuni za Usalama Barabarani. ii) Udereva wa kujihami iii) Ukaguzi wa gari kabla na baada ya safari. iv) Namna ya kukabiliana na majanga ya moto.


NB: RPC Pwani ACP Wankyo Nyigesa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ametoa onyo kwa madereva wa vyombo vya moto wote nchini wanapo ingia katika Mkoa wa Pwani watii sheria bila kusubiri kushurutishwa vinginevyo watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufutiwa leseni zao.


"Madereva wote uwe wa Polisi, magari ya serikali, magari madogo ama mabasi wote mnapaswa kutii sheria za usalama barabarani ndio maana darasa hili halina ubaguzi mpo hapa leo mkijifunza kwa pamoja"


Ameongeza hatokuwa na muhali kwa dereva atakayesababisha ajali ndani ya Mkoa wa Pwani.


Naye RTO Mkoa wa Pwani SP Mosi Ndozero ameeleza kuwa Mkoa wa Pwani umefanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 90 za mabasi na tatizo lililopo kwa sasa ni baadhi ya madereva wa magari madogo na malori kutokutii sheria za usalama barabarani hasa nyakati za usiku hivyo kupelekea ajali.


"Ajali za mabasi tumefanikiwa kuzipunguza kwa kiwango cha juu na hii imetokana na elimu tuliyowapatia madereva waliokamatwa kwa nyakati tofauti na hivyo kuwa mabalozi wetu kwa wenzao".


Ameongeza kwa kusema kuwa, kwa sasa Jeshi hilo kikosi cha usalama barabarani limeandaa mkakati kabambe wa kukabiliana na madereva wa magari madogo na malori wanaosababisaha ajali ama kufanya makosa mengine ya barabarani ambayo ni hatarishi kwa kuwakamata na kuwaingiza darasani kama ilivyo sasa kwa madereva wa mabasi ya abiria yanayoenda umbali mrefu.

No comments:

Post a Comment