Tuesday, August 20, 2019

BILIONI 1.3 ZAHITAJIKA KIBAHA KUJENGA MADARASA 65.

Na Omary Mngindo, Kibaha.
KIASI cha shilingi bill. 1.3 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 65 vya madarasa katika shule ya sekondari wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya Assumpter Mshama alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa, ambapo alisema mpango huo unalenga kuunga mkono juhudi za serikali ya kuboresha elimu, chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Alieleza kuwa kampeni hiyo iliyopewa jina la Elimisha Kibaha, ilianzishwa Aprili 25 mwaka huu na tayari imeshawafikia wadau mbalimbali wakiwemo wananchi mmoja mmoja ambao wamejitolea pesa taslimu kuanzia shilingi elfu moja na kuendelea.

"Nimewaita hapa kwa lengo la kuwaambia wa-Tanzania kuwa kampeni yetu ya Elimisha Kibaha inaendelea, tunahitaji kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 65 kwenye shule zetu za sekondari," alisema Mshama.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imetokana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari, za Kibaha Mji na halmashauri ya wilaya kufuatia ongezeko la wanafunzi kutokana na agizo la elimu bure lililotolewa na Rais Magufuli.

"Kufuatia ongezeko la wanafunzi kwa mwaka wa 2017, jumla ya wanafunzi 3,560 walifaulu, mwaka 2018 wanafunzi 3,938 na mwaka 2019 wanafunzi 4,930 ongezeko hili limechangiwa pa na wakiwemo waliohamia kutoka maeneo mbalimbali" alisema Mshama.

Alisema kuwa vinahitajika vyumba vya madarasa 65, viti 3,250 na meza 3,250 na kuwa chumba kimoja cha darasa, viti na meza kinagharimu shilingi milioni 16.5 na kwamba vyumba, meza pamoja na viti vinagharimu shilingi bilioni 1.3.

"Uzinduzi wa kampeni yetu utafanyika Agost 30, mgeni rasmi tunataraji atakuwa Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kauli mbiu yetu Kibaha 1, Mtu 1, Tofali 1, Elfu 1 kwa Roho 1," alisema Mshama.

Alimalizia kwa kutaja namba za simu na akaunti ambapo 0657,790 327, 0763961173 akaunti ya NMB 21210032409.

No comments:

Post a Comment