Thursday, August 1, 2019

WENYE ULEMAVU MSANGA WAOMBA MSAADA

Na Omary Mngindo, Kisarawe.

Wananchi wenye Ulemavu wa viungo katika Kijiji cha Msanga Kata ya Msanga wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, wanawaomba wahisani watakaoweza kuwasaidia kupata mahitaji mbalimbali.


Wakizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG kijijini hapo, wakazi hao wakijitambulisha kwa majina ya Mohamed Kom, Mwajuma Omary na Nuru Simba walisema kuwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujimudu kiuchumi.


Kom alisema kuwa wanahitaji msaada wa vyakula pamoja na makazi, na kuongeza kuwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kimaisha kutokana na kutokuwa na msaada hali inayowaweka katika mazingira magumu kiuchumi.


"Tunaishi maisha ya shida sana, huyu unayemuona kushoto kwangu ni mtoto wangu wa kike, na wale kulia ni wajukuu zangu kama unavyotuona wote tuna ulemavu wa viungo, hatuna uwezo wa kufanya jambo lolote," alisema Kom.


Kwa upande wake Mwajuma ambaye ana ulemavu wa miguu huku akiwa na watoto wawili, alisema kuwa hana msaada wowote zaidi ya mama yake mzazi ambaye nae hana mume, hali inayozidisha kuwa na maisha magumu.


"Hao watoto unaowaona ni wangu, nimezaa na mwanamme lakini amenikimbia kwa sasa msaada mkubwa unatoka kwa mama yangu ambaye nae anategemea kilimo tu," alisema Mwajuma.


Akizungumzia kuhusiana na malezi ya mtoto wake na wajukuu zake, Nuru alisema kwamba kwa sasa anaishi na baba yake mzazi ambaye ni mlemavu, sanjali na mtoto wake ambaye ni Mwajuma na wajukuu zake wawili wote wa kiume.


"Kama unavyoniona ninaishi na familia yangu ambayo wote ni walemavu wa viungo, yule ni baba yangu, Mwajuma ni mtoto wangu, na hawa ni wajukuu zangu wa kiume ambao nalazimika kulala nao chumba komoja," alisema Nuru.


Aliongeza kwamba anaishi peke yake huku akijihusisha na kilimo ambacho hata hivyo hakina tija, hali inayomuweka katika maisha magumu yeye na familia yake.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) kata ya Msanga, Pilli Mavaga alisema kuwa shirikisho lake lipo katika hatua mbalimbali za kuwasaidia ikiwemo mkopo wa asilimia 2 kutoka halmashauri.


"Kuna maombi ya mkopo wa asilimia mbili kutoka halmashauri ambayo kwa sasa tupo katika hatua ya kufungua akaunti ya shirikisho letu," alisema Mavaga.

No comments:

Post a Comment