Monday, August 5, 2019

VULU AKABIDHI KITANDA ZAHANATI YOMBO

Na Omary Mngindo.
Mbunge wa viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, mwishoni mwa wiki amekabidhi kitanda katika zahanati ya Kijiji cha Yombo Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Akiambatana na mwenyeji wake Dkt. Shukuru Kawambwa, Vulu alisema kuwa hatua hiyo inalenga kusaidia wakazi hao, ambapo mbali ya kitanda pia amekabidhi vifaa vya kutumika wakati wa kujifungua (delivery kit) na pampas za watu wazima.

Alisema kuwa akiwa mbunge wa Viti Maalum ngazi ya mkoa akishirikoana na wenzake wa majimbo wamekuwa na ushirikiano katika kusaidia kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi.

"Wananchi wenzangu leo nimekuja hapa katika zahanati yetu ya Yombo kwa ajili ya kukabidhi kitanda hiki kitakachotumika kwa wagonjwa tunaopaya huduma hii hapa," alisema Vulu.

Nae Dkt. Kawambwa alianza kwa kumshukuru Vulu kwa mapenzi aliyoyaonesha kwa wana-Yombo, kufuatia kukabidhi kitanda godoro pamoja na mifuko yenye vifaa maalumu vya kuwasitiri wagonjwa wa kike na kiume wakati wanapatiwa huduma.

"Wabunge wote kuanzia viti maalumu pamoja na wa majimbo tumekuwa tukifanyakazi pamoja katika kuwatumia wananchi wetu, kipekee nimshukuru Dada yangu Vulu kwa zawadi hii kwa wana-Yombo," alisema Dkt. Kawambwa.

Kwa upande wake muuguzi wa zamu Anna Mzeru mbali ya kumshukuru Vulu, pia amesema kwamba vifaa vilivyotolewa na mbunge huyo vina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa watano, huku akiwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia.

Mmoja wa wakazi wa Yombo Semeni Mgeni alielezea changamoto iliyopo katika zahanati yao ikiwemo upungufu wa watumishi ambapo, wapo wawili tu, hivyo kuchangia kutopatilana kwa huduma sahihi kwa muda wote.

"Utakuta mtu anakuja na mgonjwa aidha wa kuchoma sindano lakini kutokana na kuwepo kwa mtumishi mmoja pengine ndio anatoa huduma mfano ya mgonjwa aliyezidiwa anawaacha wengine anamkimbilia huyo wemgine inabidi wasubili," alisema mkazi hiyo.

No comments:

Post a Comment