Editha Karlo,Kigoma
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema
litawaadhibu wale wote watakaojaribu kuvuruga amani na usalama wa nchi.
Jeshi hilo, limetoa tahadhari kwa watu wanaotumia
mapori ya akiba vibaya kuacha kufanya hivyo.
Kauli hiyo, imetolewa
na Mkuu wa Brigedi ya Kanda ya Magharibi (202 Kikundi cha Vikosi), Brigedia
Jenerali Julius Mkunda jana, wakati wakati akiahirisha zoezi la kijeshi la
kujiweka tayari kwa wapiganaji kupambana na adui.
“Amani na usalama wa
Watanzania, lazima upewe kiupaumbele, yeyote atakayejaribu kuchezea amani
tutamshughulikia,”alisema.
Zoezi hilo ambalo lilifanyika kwenye mapori ya wilaya
za Kibondo, Kasulu na Kakonko na kupewa jina la Opereshini KIKAKA, lilikuwa la
mafanikio makubwa.
Brigedia Jenerali Mkunda alisema kumekuwa na
uharibifu mkubwa wa mapori kutumika kwa shughuli za maficho ya ujambazi,
uwindaji haramu na kilimo mambo ambayo yanafanywa na wageni kutoka nchi jirani.
“Tanzania sio shamba la bibi kwa kila
anayetaka anakuja kufanya anachojisikia, hatutakubali tutawaadhibu wote wenye
nia mbaya ya kutumia mapori yetu kwa vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria na
taratibu za nchi yetu, vinatishia amani na usalama wa raia na mali zao na
kuwafanya waishi kwa woga,”alisema
Brigedia Jenerali Mkunda.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo,
Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita kutoka Brigedi ya Kanda ya Magharibi, Kanali
Wilbert Ibuge alisema mapori yote ambayo watu wanayaona nchini yana wenyewe na
wenyewe ni jeshi hilo ambalo lina wajibu wa kuyatunza.
“Tuna wajibu wa kuyatunza mapori haya, hakuna mtu
yeyote ambaye ataingia akaachwa ayatumie anavyotaka,”alisema.
Alisema mafunzo hayo, ni sehemu ya utimamu na
utayari wa jeshi kujindaa kupambana pindi adui anapotokea na kwa sababu kwenye
vita hakuna mahali pa kufanya majaribio.
Alisema kazi ya kuwasaka na kuwakamata wote ambao
wataingia kwenye mapori hayo na kufanya vitendo vya uhalifu, itatumika kama
sehemu ya mazoezi kwa vitendo kwa wapiganaji.
Mkuu wa Kikosi
cha 24, ambacho kimesimamia na kuratibu mafunzo hayo, Meja J.S.Luhonyva
alisema mazoezi hayo yamefanikiwa kwa
kiasi kikubwa na vijana wameonyesha tayari kukabiliana na adui.
Alisema lengo la mazoezi hayo kwa kiasi kikubwa
limefikiwa medani zote za mapambano ya kivita.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kigoma,Brigedia
Jenerali mstaafu Emanuel Maganga, Mkuu wa Wilaya Kasulu, Kanali Simon Hanange
alisema mazoezi hayo yatasaidia mkoa kuendelea kuwa na aman muda wote.
No comments:
Post a Comment