Tuesday, August 6, 2019

RAS LINDI ATAKA UDHIBITI WA RISITI VITUO VYA MAFUTA.

Hadija Hassan, Lindi.

Kutokana na Mfumo wa Mashine za kielektroniki (EFD) zilizofungwa katika vituo vya Mafuta hapa Nchini kutoa Lisiti ambazo hazina majina ya wateja wanaopatiwa Huduma, Katibu tawala wa Mkoa wa Lindi , BI, Rehema Madenge amewashauri Wamiliki wa Vituo vya Mafuta kuhakikisha risiti wanazozalisha hazibaki hovyo ili kuwadhibiti watu wenye nia ovu wanaofanya udanganyifu.

Madenge alitoa ushauri huo jana alipotembelea katika Banda la Maonesho la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Lindi katika Maonesho ya 27 yanayofanyika Kanda ya Kusini katika Viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi.

Alisema wapo baadhi ya Madereva wanaofanya ujanja ujanja wa hela za Mafuta wanazopewa na Ofisi zao ambao sio waaminifu wanatumia risiti wanazozikuta katika vituo vya mafuta kulinganisha na fedha walizopewa ofisini kwao.

Alisema ili kudhibiti hali hiyo ni vyema wamiliki hao wa vituo vya mafuta kufanya udhibiti wa risiti wanazozalisha pasipo kuwapa wateja wanaowahudumia pamoja na kuwataka wateja wote wanaokwenda kupata huduma katika vituo hivyo kuchukuwa risiti zao mara baada ya kuhudumiwa.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evod Mmanda ambae alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Pili ya Maonesho ya Nane nane kanda ya kusini 2019 alitoa wito kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwadhibiti pamoja na kuwasimamia mawakala wa mashine hizo za Kielektronik (EFD) kupeleka mashine hizo kwa wafanya biashara kwa wakati.

Mmanda alisema Mamlaka hiyo haina budi kukabiliana na upungufu wa mashine hizo huku akisisitiza usimamizi wa karibu ili kuondoa changamoto hiyo ya upungufu wa mashine.

No comments:

Post a Comment