Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu, akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi, Wilaya ya Siha, Mkoa wa
Kilimanjaro alipokuwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.
...................................
Na Veronica Simba – Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
ametoa onyo kali kwa Mkandarasi Urban & Rural Engineering, ambaye
anatekeleza mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mkoani Kilimanjaro, kwa
kumwambia asiijaribu serikali kwa kutikisa kibiriti kwani njiti zimejaa na kitawaka.
Alitoa onyo hilo kwa nyakati tofauti
Agosti 25, 2019 akiwa katika ziara ya kazi kwenye Wilaya za Hai na Siha, baada
ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wao kuwa kasi ya
mkandarasi huyo hairidhishi.
Akizungumza katika mkutano na wananchi
wa Hai, Naibu Waziri Mgalu alikiri mbele yao kuwa utendaji kazi wa mkandarasi
husika unasuasua na zaidi ameonesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa serikali
kwa kutoitikia wito alipoitwa kushiriki kwenye ziara hiyo pasipo kutoa sababu
yoyote.
Akielezea zaidi, Naibu Waziri alisema
yeye binafsi alijaribu kuwasiliana na mkandarasi huyo kwa njia ya simu pasipo
mafanikio na hata ujumbe mfupi wa maandishi aliomtumia kumtaka apokee simu,
haukujibiwa; kitendo ambacho alikiita ni dharau.
“Sasa mimi nataka nitoe salamu kwake.
Mkandarasi Urban & Rural Engineering naona unatikisa kibiriti, unataka ujue
kama kina njiti au hakina, na kama njiti zimejaa au zina baruti. Nataka
nikwambie kibiriti kimejaa, njiti zina baruti na kitawaka.”
“Ulichokifanya ni dharau na unatupelekea
tufanye maamuzi ya kuanza mapitio; na ni kweli nathibitisha ameshindwa kazi,”
alisema Naibu Waziri.
Kufuatia hali hiyo, alimwagiza
Msimamizi wa Mradi husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumjulisha
mkandarasi huyo kwenda Dodoma mara moja kushiriki katika kikao kitakachofanya
mapitio ya suala hilo ili ikibidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
“Kama ameshindwa kazi, tutawapatia
wakandarasi wengine au hata TANESCO wanaweza kumalizia kazi husika.”
Awali, Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, alimweleza Naibu Waziri kuwa, Mradi wa
Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Kilimanjaro unagharimu kiasi cha shilingi
za kitanzania takribani bilioni 12.
Alisema, Mradi unahusisha ujenzi wa
kilomita 150 za msongo wa umeme wa kilovoti 33, ujenzi wa kilomita 334 za
msongo wa umeme wa kilovoti 400 na ufungaji wa mashine umba (transfoma) 132 na
kwamba unatarajiwa kuunganishia umeme jumla ya wateja 3,572 katika vijiji 75
ndani ya mkoa.
Aliongeza kuwa, kwa ujumla
utekelezaji wa mradi husika mkoani humo umefikia asilimia 43 hadi sasa.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri
aliwasha umeme katika shule za msingi za Roo na Msamadi zilizopo wilayani Hai,
pamoja na eneo la viwanda Mwangaza na shule ya msingi Gararagua wilayani Siha.
Pia, alizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi wilayani Siha.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
akiwasha rasmi umeme katika shule ya msingi Gararagua, iliyopo wilayani Siha,
Mkoa wa Kilimanjaro akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.
Umati wa wananchi wakishuhudia tukio
la uwashwaji rasmi wa umeme katika shule ya msingi Msamadi iliyopo wilayani
Hai, Mkoa wa Kilimanjaro. Tukio hilo lilifanywa na Naibu Waziri wa Nishati,
Subira Mgalu (hayupo pichani), akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.
No comments:
Post a Comment