Kamishina
wa Uraia na Pasipoti kutoka Idara ya Uhamiaji Gerald Kihinga.
.....................................
Na Said
Mwishehe, Michuzi TV
IDARA ya Uhamiaji imesema inamshikilia Mwandishi
Erick Kabendera na kwa sasa wanaendelea kuchukua taarifa zake kuhusu uhalali wa
uraia wake.
Kamishina wa Uraia na Pasipoti kutoka Idara ya
Uhamiaji Gerald Kihinga amesema wanamshikilia Kabendera ili kujiridhisha na
uraia wake na huo ni wajibu wao pale wanapokuwa na mashaka na uraia wa mtu.
"Idara ya Uhamiaji ilipata taarifa kutoka kwa
wasamaria wema kuhusiana na utata wa uraia wa Erick Kabendera mwenyewe alikua
hajawahi kuhojiwa kuhusiana na uraia wake, kwa kuwa hakufika ofisini pamoja na
kumtumia wito mara kadhaa wa kumtaka afike ofisini kwa mahojiano.
"Na ndio maana sasa idara ya uhamiaji kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi imeweza kumtafuta na kumkamata mhusika ili
aweze kuhojiwa kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi kuhusiana na uraia
wake.Uchunguzi utakapokamilika, matokeo ya uchunguzi huo
yatatolewa,"amesema Kamishna Kihinga.
Amefafanua ieleweke kuwa uchunguzi wa utata wa
uraia umekuwa ukifanyika kwa watu mbalimbali wakiwemo watu mashuhuri katika
jamii.
Hivyo suala hilo limeibua hisia huenda kwa kuwa mhusika ni mwanahabari.
Amesisitiza Idara ya uhamiaji imekuwa ikishirikiana
na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama katika utekelezaji wa majukumu yake
mbalimbali , kwa hiyo hilo sio suala geni.
Hata hivyo idara hiyo imetoa mwito kwa jamii
kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa mbalimbali ya kiuhamiaji ili kuhakikisha
nchi yetu inaendelea kuwa salama.
Baada ya taarifa hiyo waandishi wa habari
kutoka vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania vilitaka kufahamu
atashikiliwa kwa muda gani na kwa taarifa za awali Kabendera anahusishwa na
uraia wa taifa gani.
Kamishina Kihinga amejibu wataendelea kumshikilia
hadi pale watakapokamilisha taarifa wanayoihitaji na kuhusu taifa gani
anahusishwa nalo hilo kwa sasa bado kwani ndio wanaendelea kukusanya taarifa.
Alipoulizwa Kabendera amekamatwa na nani? Amejibu
amekamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Alipoulizwa
kwanini waliokwenda kumkamata hawakutaka kutoa vitambulisho na walikuwa wamevaa
kiraia, amejibu wana mbinu nyingi za kumkamata mtu ambaye ameitwa na kisha
akakaidi.
Hivyo waliamua kutumia mbinu ya kutovaa sare za uhamiaji.
No comments:
Post a Comment