Thursday, August 15, 2019

PANDE NA MLINGOTINI WAMTAKA JPM

Na Omary Mngindo, Bagamoyo

WAKAZI wa vijiji vya Pande na Mlingotini Kata ya Zinga wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamemuomba Rais Dkt. John Magufuli afike kutoa tamko linalohusiana na hatma yao kuhusu ujenzi wa bandari.


Wakazi hao wametoa rai hiyo katika mkutano ulioandaliwa na mbunge wa jimbo hilo Dkt. Shukuru Kawambwa, ambae yuko kwenye ziara ya kutembelea kata za jimbo hilo, akipokea changamoto, maoni na ushauri atakazozifikisha kwa mawaziri bungeni jijini Dodoma.


Wakizungumza kwenye kijiji cha Pande, wakazi Ramadhan Wading'ola alisema kuwa wamechoshwa na sintofahamu hiyo, inayohusiana na kutakiwa kuhama kijiji kizima kupisha mradi huo, ambao mchakato wake bado unaendelea.


"Tumechoshwa na hii sintofahamu ya mradi wa bandari, ambao kwa sasa una miaka saba, tunakuomba mbunge Kawambwa tuletee Rais Dkt. John Magufuli aje atoe tamko kuwa tukae au tuhame," alisema Mzee Wading'ola.


Aliongeza kwa kusema kwamba mara nyingi wanamuona Rais Magufuli katika tv akitoa tamko la kuwasaidia wanyonge, ikiwemo la shamba la Magereza hivyo wanamtaka afike katika vijiji vyao lakini hapa kwetu mbona haji? au haoni mateso yetu?," alihoji.


Salum Issa alisema kuwa kwa sasa hawauhitaji tena mradi huo, badala yake waachwe waendelee na makazi yao, kwani katika eneo hilo wana huduma zote za kijamii.


"Tunakushukuru mbunge kama jina lako lilivyo kwa kutuombea kuendelea kukaa, lakini kuna notisi nyingine isiyo rasmi ya wafugaji ambao wameingia kwa wingi katika eneo tulilotakiwa kwenda, muda wote wapo kwenye mashamba,"alisema.


Kwa upande wake Matata alisema kuwa kama hakutopatikana ufumbuzi wa suala hilo, hawapo tayari kushiriki chaguzi zinazokuja kuanzia za uenyekiti, udiwani na ubunge na rais mwakani.


"Hapa shuleni tulipo kuna eneo kubwa la mkutano utaokuwa chini ya Rais wetu Magufuli ambae ni rais wa wanyonge, kamlete huyo baba aje hapa," alisema Matata.


Nae Mama moja ambaye hakujitambulisha jina alisema kwamba wamechoshwa na vipigo kutoka kwa wafugaji ambao wanalisha katika mashamba, huku wakishambulia wananchi, hivyo amemtaka Dkt. Kawambaa afanyie kazi malalamiko yao.


Akizungumza na wananchi hao Dkt. Kawambwa aliahidi kuyabeba na kumfikishia Rais ili kuona ni namna gani anavyoweza kulipatia ufumbuzi.


"Mimi ni mtumishi wenu, nimepokea changamoto zenu nitaziwasilisha kwa Rais tuone kama atakuwa na nafasi anaweza kuja, tukumbuke Dkt. Magufuli anaiongoza serikali ya watu wanyonge," alimalizia Dkt. Kawambwa.

No comments:

Post a Comment