Saturday, August 3, 2019

MWENYEKITI WA CCM LIWALE AFIKISHWA MAHAKANI KWA TUHUMA ZA KUPOKEA RUSHWA.

Na Hadija Hassan, Lindi.


Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi imemkamata na kumfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Likongowele Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi Mohamedi Nandope kwa Tuhuma za Kuomba na kupokea Rushwa.


Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Mkutano wa Taasisi hiyo Mjini Lindi jana, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa huo, Noel Mseo alisema Nandope alikamatwa tarehe 28/07/2019 majira ya saa moja jioni mtaa wa Nangando Wilayani Liwale kwa tuhuma za kupokea Rushwa kutoka kwa Mtumishi wa Idara ya Afya wa Wilaya hiyo.


Mseo aliwaeleza wanahabari kuwa Taasisi hiyo ilipata taarifa kutoka kwa Raia mwema ya kuwepo kwa mazingira ya kiongozi huyo wa chama cha Mapindizi CCM kuomba Rushwa ambapo ilianza kufuatilia kwa ukaribu na kubaini kuwa Kiongozi huyo alikuwa anashawishi kupewa Rushwa.


Alisema baada ya hapo Taasisi hiyo iliamua kumuwekea Mtego ambapo Mshitakiwa aliweza kufika Eneo la Tukio ambalo walikubaliana na Muhudumu huyo wa Afya na hatimae wakaweza kumnasa akiwa na fedha Taslimu ambazo Tsh. 300,000. ambazo alikuwa ameziomba kwa Mtumishi huyo.


Mseo Alidai kuwa mwenyekiti huyo alikuwa anaomba fedha kutoka kwa mtumishi huyo wa idara ya afya kwa madai kwamba angeweza kumsaidia ili asichukuliwe hatua kutokana na tuhuma za malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya utoaji huduma Dhidi yake.


Hata hivyo Mseo alidai kwamba Taasisi hiyo tayari imeshamfikisha Mahakama ya Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi Mtuhumiwa huyo ambapo kesi yake itatajwa Tarehe 12/08/2019

No comments:

Post a Comment