Na
Omary Mngindo,
WAKAZI
wa Kitongoji cha Umakondeni Kijiji cha Kongo Kata ya Yombo, wilaya ya Bagamoyo
Mkoa wa Pwani, wameomba wapelekewe Mhandisi wa ujenzi kuangalia uwezekano wa
kujenga daraja katika mto Ruvu unaopita eneo lao.
Wakazi
hao wametoa kilio hicho mbele ya mbunge Dkt. Shukuru Kawambwa, kwenye ziara ya
kikazi jimboni humo, ambapo akiwa kijijini hapo wakazi hao walisema kuwa
wanaliwa na mamba kutokana na kuvuka ng'ambo ya pili kwa ajili ya kilimo.
Aidha
wamelalamikia gharama za kuunganishiwa maji, ambapo walisema kwamba pamoja na
kuishi ndani ya eneo la mradi ulioko kijijini hapo, lakini gharama ya huduma
hiyo kwa bomba yenye urefu wa mita 50 wanatakiwa walipie shilingi laki mbili.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake, Ally Jasilii alisema kuwa wanalima ng'ambo ya mto Ruvu
chini ambapo kila siku wanavuka kwemda na kurudi, hali inayowaweka katika
wakati mgumu huku akieleza kwamba kuna wenzao wameliwa au kujeruhiwa na mamba.
"Mheshimiwa
Mbunge tunakuomba utuletee Mhandisi aangalie uwezekano wa kujenga daraja katika
mto Ruvu chini, sisi tegemeo letu ni kilimo ng'ambo ya mto, wenzetu wameliwa na
kujeruhiwa na mamba, tuletee Mhandisi," alisema Jasilii.
Kwa
upande wake Ibrahimu Issa alisema kuwa wanakabiliwa na hatari ya mamba kutokana
na kutegemea maji ya mto huo, pamoja na wao kuishi ndani ya mradi wa mradi
lakini hawana huduma hiyo.
"Tunaambiwa
kuunganishiwa bomba yenye urefu wa mita 50 shilingi laki mbili, mimi nina ardhi
eka 3 sasa hizo mita zao 50 si zitaishia shamba la jirani yangu, tunakuomba na
hili ukalifanyiekazi," alisema mkazi huyo.
Akijibia
malalamiko hayo, Dkt. Kawambwa alisema kuwa amepokea malalamiko hayo na kuahidi
kuyafanyiakazi, huku akisema kuwa ujenzi wa daraja mto huo unawezekana, huku
akisema lakini kazi yake ni kubwa.
"Pamoja
na kwamba ujenzi wa daraja mto Ruvu kazi yake ni kubwa, lakini hakuna
lisilowezekana, nitakwenda kuzungumza na Wahandisi tutakuja kuangalia uwezekano
wake," alisema Dkt. Kawambwa.
Akizungumzia
kilio cha gharama ya kuunganishiwa maji, Dkt. Kawawambwa alisema kuwa kimsingi
wakazi wanaoishi ndani ya eneo la mradi kungekuwa na unafuu wa bei, na kwamba
kwa namna moja au nyingine wanasaidia kulinda miundombinu ya mradi.
"Haya
yote nimeyapokea nitakwenda kukutana na viongozi husika kuzungumza nao hatimae
kuwapatia mrejesho baada ya mazungumzo yetu, kuhusu mhandisi nitakuja nae kuona
namna itakavyowezekana," alimalizia Dkt. Kawambwa.
No comments:
Post a Comment