Friday, August 30, 2019

UHABA WA KONDOM LINDI, MADIWANI WAPAZA SAUTI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Mkoani humo wametaka kufahamu sababu ya kuadimika kwa Kondomu katika Halmashauri yao Madiwani hao walihoji hilo, wakati wa kikao cha Baraza kupitia na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kamati mbalimbali, ikiwemo ya Ukimwi katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo uliopo mjini Lindi.

Miongoni mwa wajumbe wa Baraza hilo waliotaka kufahamu sababu za kutopatikana kwa zana hizo muhimu katika maeneo mbali mbali ya Halmashauri yao ni Diwani wa Kata ya Namangale, Sudi Kanduru (CCM).

Kanduru alisema amelazimika kuuliza Swali hilo kutokana na kupokea malalamiko kutoka kwa Wananchi wa kata yake ambapo alidai kuwa hata hivyo alifanya uchunguzi katika baadhi ya maeneo hayo na kubaini kuwepo kwa ukweli juu ya malalamiko ya wakazi wake.

Hoja hiyo ya Kanduru liliungwa mkono na madiwani wenzake akiwemo Mohamedi Mkulyuta {Kiwalala}, Halima Mwambe (Rondo) na Hassani Kunyong’onyea (Mtama) ambapo kwa pamoja walishauri jitihada za makusudi na haraka zifanyike zipatikane Kondomu ili kunusuru Afya za Jamii zao.

Nae Hasani Kunyongonyea Diwani wa Kata ya Mtama (CHADEMA) alisema iwapo jitihada za upatikanaji wa zana hizo hautaharakishwa kuna hatari kubwa ya idadi ya wananchi kuathirika na maambukizi ya VVU pamoja na magonjwa mengine ya Zinaa katika Wilaya hiyo.

Akijibu madai ya Madiwani hao, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Samweli Gunzari amewaondoa hofu wananchi kupitia wawakilishi wao kwa kusema anatambua uwepo wa upungufu wa zana hizo na kueleza Serikali inalifanyia kazi ili ziweze kupatikana ili jamii iweze kuzitumia.

No comments:

Post a Comment