Monday, August 19, 2019

VULU AWAASA WANA-CCM KISIJU.

Na Omary Mngindo, Mkuranga.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Zaynab Matitu Vulu, amewaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mkuranga mkoani hapa, kutofanya makosa katika uchaguzi wa serikali za vijiji na Vitongoji, utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Mbunge huyo ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki akiwa Kisiju, akiambatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (MNEC) Haji Abuu Jumaa, wakielekea Kisiwa cha Koma, ambapo akiwa huko Vulu alikabidhi kitanda na mashuka ikiwa ni ahadi yake kwa wananchi hao.

Akiwa Kisiju Vulu alipata fursa ya kuzungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho na Mabaraza ya Jumuiya za Kata, kwenye kikao maalumu, mbele ya MNEC Haji, ambapo alianza kwa kuwashukuru kwa kuendelea na majukumu yao ya kukiimarisha chama hicho.

"Kwaniaba ya viongozi wa chama ngazi zote, nianze kwa kuwashukuru na kuwapongeza kutokana na umoja wetu wa kuendelee kukiimarisha chama chetu, pia niwaombe tuondokane na yale yaliyosababisha kushindwa kwenye chaguzi zilizopita, nadhani tunayatambua," alisema Vulu.

Aidha aliwataka wanachama hao kuyasena mazuri yanayotekelezwa kwa vitendo na Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, ikiwemo miradi mikubwa inayoendeea kila kona ya nchi, ambapo kuna iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa.

"Kuna miradi mingi imefanyiwa kazi katika kila kona ya nchi, kuna iliyokamilika na inayoendelea kukamilishwa, tuwe mstari wa mbele kuyazungumzia hayo, kwani yanaonekana wazi, hivyo hatuna sababu ya kutoyasemea," alisema Vulu.

Vulu amempongeza MNEC Haji kwa ziara hiyo ya kusikiliza changamoto, kuzipokea kisha kuzifikisha kwa viongozi ngazi za juu ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowagusa wananchi, huku akimpongeza Mbunge wa jimbo hilo Abdallah Ulega.

Kwa upande wake MNEC Haji aliwaambia wanachama hao wa Kisiju kuwa, ziara hiyo ya kutembelea Kata zote mkoani Pwani madhumuni yake ni kukutana na viongozi wanaokisimamia chama hicho ngazi za vijiji ambao ndio msingi imara ndani ya chama.

No comments:

Post a Comment