Na Veronica Simba – Dodoma.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa idadi ya
wanaounganishiwa umeme vijijini kupitia miradi mbalimbali inayoendelea ni ya
awali na itakuwa ikiongezeka kadri wananchi husika watakavyokuwa wakilipia
gharama yake ambayo ni shilingi 27,000 tu.
Alieleza hayo leo, Agosti 20, 2019
jijini Dodoma, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na wajumbe kadhaa wa Kamati
hiyo walioonesha wasiwasi wao kuwa idadi ya wananchi wanaounganishiwa umeme
vijijini ni ndogo.
“Kinachofanyika hivi sasa ni kupeleka
miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali vijijini na kuunganisha wateja wa
awali, Wengine wataendelea kuunganishwa kwa wakati wao kadri wanavyolipia,”
alifafanua Waziri.
Aidha, kuhusu agizo la serikali kwa
wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kutumia vifaa vya ndani ya
nchi, Waziri ameieleza Kamati husika kuwa msimamo huo unatokana na matumizi ya
vifaa vya ndani kuwa na tija zaidi kuliko vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.
Akifafanua, alieleza kuwa kuagiza
vifaa nje ya nchi ni gharama kubwa ukilinganisha na kutumia vifaa vya ndani.
Pia, alisema, ni rahisi zaidi kwa
serikali kusimamia na kudhibiti ubora wa vifaa vya ndani kuliko
vinavyotengenezwa nje ya nchi.
Aidha, aliongeza kuwa muda unaotumika
kupata vifaa vinavyotengenezwa ndani ya nchi tangu siku vinapoagizwa ni mdogo
kulinganisha na ule unaotumika kuagiza na kuletewa vifaa hivyo kutoka nje ya
nchi.
Waziri pia alizungumzia katazo
lililotolewa na serikali kuhusu wananchi vijijini kulipia nguzo ambapo alisema
uamuzi huo ulifikiwa ili kuwapunguzia gharama wananchi hao ambao wengi kipato
chao ni kidogo.
“Kwa uhalisia, umeme vijijini
unatolewa bure kwa wananchi na gharama zake kuchukuliwa na serikali.
Hata hiyo 27,000 wanayolipa ni
gharama za ushuru wa thamani tu ambayo ni asilimia 18 ya gharama husika.
Sasa ukimlipisha mwananchi huyo nguzo
itarudisha tatizo palepale, hivyo nasisitiza tena kwamba wananchi wa vijijini
hawatakiwi kulipia nguzo.”
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, ameieleza
Kamati hiyo kuwa, tangu kuanzishwa kwake, REA imetekeleza miradi mbalimbali
ikiwemo Miradi ya Awali, Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Kwanza (REA
I), Awamu ya Pili (REA II) na Awamu ya Tatu (REA III).
Alisema kuwa kukamilika kwa miradi
hiyo mwaka 2021, kutawezesha vijiji vyote 12,268 vya Tanzania Bara kufikiwa na
miundombinu ya umeme.
Katika kikao hicho, Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini ilikuwa ikipokea taarifa ya maendeleo na
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya REA pamoja na changamoto inazokabiliana
nazo.
Wengine walioshiriki kikao hicho ni
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Haji Janabi
pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
No comments:
Post a Comment