Monday, August 12, 2019

NDOA ZA KIISLAMU, KIKRISTO, BOMANI SASA KUSAJILIWA OFISI YA MKOA


Mkuu wa mkoa wa Daresalaam, Paul Makonda amesema yuko kwenye mpango wa kutaka kusajili ndoa zote zinazofungwa katika mkoa wa Daresalaam, dhamira ikiwa ni kuwasaidia wanawake ambao wanalaghaiwa na wanaume wapate nusra.

Makonda ametangaza nia hiyo mapema hii leo wakati akizungumza na waandishi wa habari.


Amesema watasajili ndoa zote kuanzia zile za Kiislamu ambazo dini yake inaruhusu kuoa wanawake wanne, lakini pia ndoa ya kikristo ambayo inaruhusu mwanamke mmoja na ile ya bomani.

Amesema baada ya ya kukamilika kwa ugeni wa SADC, wataanza mchakato wa majadiliano ili kuangalia njia nzuri ya kuondoa udanganyifu wa wanaume.

"Hili sio suala la Makonda peke yake, tutajadiliana na wadau ili kuona namna tutakavyoliweka, lakini natamani kuleta furaha miongoni mwa wanawake, huwezi ongoza watu ambao hawana furaha, lazima tuangalie namna ya kuwasaidia," alisema Makonda

Amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kukutana na wadada wote wa mkoa huo, walioumizwa baada ya kuahidiwa kuolewa na kisha mwanaume kuingia mitini na kuangalia ni njia gani nzuri zaidi ya kuwaokoa na janga hilo.

Makonda  amedai ya kwamba amekuwa akikutana na malalamiko mengi sana kutoka kwa wadada wa mkoa huo kwamba wamechoka kutapeliwa.

''Tunaompango mzuri tu wa kukutana na wadada walioumizwa,  huwezi kuwa kiongozi afu unaongoza watu walioumizwa na kutapeliwa na vijana ambao wanaona raha tu, tunataka tufikie hatua mtu akioa anaandika kwenye database ya mkoa,  ili mwanamke akitaka kuolewa anaangalia huyu jamaa kaoa au hajaoa'' amesema Makonda.

Makonda ameongeza kuwa,  wanaoumizwa wengi ni kina dada kwa sababu wanawake wakipenda huwa wanapenda kweli na wao kuwa wahanga wakubwa wa matapeli.

Amesema mkutano wa SADC wanataka kuutumia kujifunza mambo mbalimbali,  ikiwemo suala la wadada kutapeliwa juu ya masuala ya ndoa, kwa kuangalia nchi zingine zinashughulika vipi na masuala hayo

No comments:

Post a Comment