Serikali kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kutekeleza mradi wa
ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Ufundi cha
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Hayo yamesemwa Wilayani Karagwe na
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha katika ziara ya
kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu katika wilaya
hiyo, ambapo amesema lengo la kutekeleza mradi huo
ni kuongeza udahili wa wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi.
Ole Nasha amesema serikali imeweka
mkakati wa kukarabati na kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya, kwani ili
kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kama nchi kuwa na vijana wenye maarifa na
stadi mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kushiriki
katika uchumi wa viwanda.
“Rais ameweka nguvu nyingi katika
kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali
zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi
yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo
mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.
Wakati huo huo, Naibu Waziri ametoa
miezi mitatu kwa wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha wanamaliza ujenzi
na ukarabati wa chuo hicho, ambapo amesema hajaridhishwa na sababu zilizotolewa
na mhandisi msanifu kutoka TBA zilizopelekea kutokamilika kwa mradi kwa wakati.
Ole Nasha anesisitiza kuwa hakuna
wakati wowote ambao fedha iliyopaswa kutolewa imeshindwa kutolewa na VETA kwani
mpaka sasa TBA imeshalipwa zaidi ya shilingi bilioni moja ambayo ni asilimia 25
ya fedha yote iliyopaswa kulipwa wakati ujenzi umefikia asilimia 44 tu.
Awali Mhandisi Msanifu wa Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), Kelvin Joas alimweleza Naibu Waziri kuwa kutokukamilika
kwa mradi huo kwa wakati nikutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo
za kimkataba na kuwapelekea kuomba kuongezewa muda wa miezi sita baada ya muda
wa mkataba kuisha Julai 26,2019.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya, Godwin Kitonka amesema Halmashauri yake inaishukuru
serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutenga fedha zaidi
ya bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ambayo ni pamoja na jengo la
utawala, ukumbi mdogo, vyoo vya nje, bweni la wasichana na kukarabati karakana
ya ushonaji na uchomeleaji chuma.
Mwanafunzi Masau Josephat,
ameishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia
pamoja na kuongeza majengo ambayo awali hayakuwepo kwani mwanzoni hayakuwa
yakiidhisha, huku wakiiomba serikali kuongeza baadhi ya kozi ambazo
hazipatikani chuoni hapo ili kupanua wigo wa upatikanaji wa maarifa na stadi
kwa vijana wa Karagwe na maeneo ya jirani.
No comments:
Post a Comment