Na Hafsa Omar, Katavi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani ametoa agizo kwa vyombo vya usalama mkoani Katavi kuwakamata
wakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza umeme vijijini mkoani humo kutoka
kampuni ya CRCBEG baada ya kusuasua katika utekelezaji wa kazi.
Alitoa agizo hilo jana Agosti 25,
2019 wakati akielekea kwenye kijiji cha Ntibiri wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi
ili kukagua kazi ya usambazaji umeme, mara baada ya kuwasha umeme katika kijiji
Kirida wilayani humo.
Waziri wa Nishati pia alitoa agizo la
kushikiliwa kwa hati za kusafiria za wakandarasi hao mpaka watakapomaliza kazi
zao za usambazaji umeme walizopangiwa na Serikali.
“ Nilitoa mwezi mmoja eneo lote la
kilometa 27 muwe mmeshawasha umeme lakini bado, Kijiji cha Majimoto bado
hamjawasha, leo nimepita hapa sijaona vibarua wakihangaika, na wala nguzo
hazijafika, nimefika Shule ya Sekondari kule nguzo hazijafika na wala
hamjasambaza popote.”alisema Dkt. Kalemani.
Waziri Kalemani, pia aliwaagiza
Mameneja wa TANESCO kutoondoka katika eneo hilo ili kuhakikisha kazi ya
usambazaji umeme inafanyika kwa kasi zaidi, “ninataka umeme ufike Kijiji cha
Majimoto, ifikapo tarehe 5 mwezi ujao na mameneja wote mtabaki hapa kusimamia
kazi.”
Akizungumza na Wananchi wa kijiji cha
Ntibiri, Dkt.
Kalemani aliwaeleza wananchi hao kuwa, Serikali imetoa kiasi cha
shilingi bilioni 89 kwa ajili ya usambazaji umeme mkoani Katavi na
kuwahakikishia kuwa, mkoa mzima utapata umeme.
“Leo nimetoa maelekezo kuwa, eneo la
Ntibiri na maeneo ya jirani, wakandarasi watamaliza kazi mwezi wa 12 mwaka huu,
hakuna kijiji kitakachobaki, sasa kama eneo lako halijapitiwa na umeme, kuanzia
sasa litapitiwa.” Alisema Dkt Kalemani.
Akiwa wilayani Mlele, Waziri wa
Nishati, pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Society katika eneo la wachimbaji
wadogo wa dhahabu hali itakayopelekea wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa
tija.
No comments:
Post a Comment