Sunday, August 27, 2023

LATRA YAIAHIDI KAMATI YA BUNGE KUBORESHA SHUGHULI ZA USAFIRISHAJI, YATOZA FAINI MABASI SH. MIL.1, 250,000/-


 MKURUGENZI Mkuu  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo, ameihakikishia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha shughuli za usafirishaji nchini na kuwapima madereva ili waendeshe vyombo vya moto kwa usalama zaidi.

Suluo aliyasema hayo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Miraji Mtaturu, kuipongeza LATRA
kwa kusimamia mfumo utoaji wa tiketi kwa mtandao ambao umeanza kupunguza kero kwa abiria.


” Tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ukamilifu na kuufanyia kazi
ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa lengo la kuboresha shughuli za usafirishaji ikiwemo kuendelea kuwatahini madereva ili kuhakikisha
abiria wanasafiri kwa usalama,”. alisema Suluo wakati akiwasilisha taarifa ya
mamlaka hiyo kwa wabunge wa kamati hiyo Agosti 25, 2023.
 


LATRA katika kuhakikisha inadhibiti mawakala wa mabasi wanaokwepa kukata tiketi kwa mfumo wa mtandao,  LATRA Mkoa wa Singida juzi iliyatoza faini ya Sh. 250,000 kila basi kwa mabasi matano na kuvuna jumla ya Sh. 1, 250,000.


Mabasi yaliyotozwa faini hizo ni ya Kampuni ya Nyahunge mabasi manne na
basi moja la kampuni ya Supafeo ambapo mabasi hayo yalikumbana na adhabu hiyo kutokana na  kuwakatia abiria tiketi za zamani ambazo sio za kielektroniki  zilizopigwa marufuku.


Hatua ya LATRA Mkoa wa Singida  kuyatoza faini mabasi hayo ilikuja baada
ya mmoja wa wasafiri waliokuwa ndani ya mabasi hayo kutoa taarifa kwa Afisa
Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida, Layla Dafa kuwepo kwa abiria waliokatiwa tiketi ambazo sio za
kielektroniki.


Baada ya Dafa kupewa taarifa hizo, alimtuma Afisa wake aitwaye Kilua Mbezi kuyafutilia  mabasi hayo Stendi Kuu ya Mabasi Mkoa wa
Singida ya Misuna na kubaini kosa hilo na kuyatoza faini.


Abiria waliokuwemo kwenye moja ya mabasi hayo walimpongeza Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida kwa kulifanyia kazi suala hilo kwa haraka na waliomba kuendelea na moto huo wa kazi hasa pale wanapopata taarifa kutoka kwa abiria na kuchukua hatua kwa haraka kama
walivyofanya kwani mara nyingi katika maeneo mengine maafisa hao huwa hawafiki eneo la tukio jambo linalowakatisha tamaa na kuendelea kukithiri kwa vitendo hivyo.
 


Afisa wa LATRA Mkoa wa Singida Kilua Mbezi baada ya kuyatoza faini mabasi
hayo alitoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu na faida ya kupatiwa tiketi za mtandao na kuwa kabla ya kupanda gari nilazima wapatiwe tiketi hizo na kama
watawakatalia na kuwapa za zamani ambazo zimepigwa marufuku watoe taarifa kwa kupiga namba ya bure 0800110020.


Mbezi pia aliwakumbusha wafanyakazi wa mabasi hayo kuendelea kufuata sheria za usafirishaji ili kuepuka adhabu mara watakapobainika kutenda makosa na kuwa jambo hilo lipo ndani ya uwezo wao na kuwa wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu hiyo. 


Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Miraji Mtaturu akizungumzia baadhi ya faida za mfumo wa ukataji wa tiketi kimtandao (Kielektroniki)  alisema ni pamoja na kupunguza mianya ya uvujaji wa mapato kwani abiria ana uhuru wa kukata tiketi basi analolitaka na  mmiliki wa basi anaona idadi ya siti zilizokatwa tofauti na zamani na kuwa faida hizo zipo kwa wahusika wote, abiria, wafanyakazi wa mabasi hayo  mmiliki na Serikali.


Tunawapongeza sana LATRA
sababu kupitia mfumo wa tiketi mtandao abiria anaweza kukata tiketi akiwa
popote bila kulanguliwa na mawakala , lakini pia mfumo huu umerahisisha
ukusanyaji wa mapato kwa wamiliki na Serikali sababu unaweza kuona idadi za
tiketi moja kwa moja kupitia mfumo,’’ alisema Mtaturu.


Mara baada ya mfumo wa Tiketi Mtandao kuanza kufanya kazi rasmi Julai 1, 2022, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilifanya mkutano na wadau wa usafirishaji kutathmini utekelezaji wa mfumo huo na kujadili changamoto zinazojitokeza ili kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na ukataji wa tiketi kimtandao.


No comments:

Post a Comment