Sunday, August 20, 2023

BUSH LAWYER AFICHUA SIRI YA BARAZA LA MAASKOFU WA KANISA KATOLIKI KUPINGA MKATABA WA BANDARI.

 

Na Mwandishi Wetu.


IKIWA ni siku moja tu tangu Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) wakutame jijini Dar es Salaam na kutoa tamko lao kupinga mkataba wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Mussa Chengula maarufu ‘Bush Lawyer’ ameibuka na kufichua siri ya kupinga mkataba huo.



Akizungumza na waandishi wa habari jana Agost 19/2023 jijini Dar es Salaam, Chengula amewataka wakosoaji wa mkataba wa Bandari kuacha kujificha kwenye kichaka cha mkataba ilihali wana jambo jingine lililojificha dhidi ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.



Chengula maarufu kwa jina la ‘Bush Lawyer’ amedai viongozi wa dini wamekuwa ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa ubadhirifu unaoikosesha serikali mapato yanayotokana na bandari yetu hiyo.


 “Baadhi ya viongozi maarufu na makundi ya kijamii wakiwemo wanasiasa, wafanya biashara na wakubwa na baadhi ya viongozi wa Dini walijituma kwa maslahi yao binafsi na kutumika kwa maslahi ya washirika wao binafsi na kugeuza Bandari yetu kuwa shamba la bibi kwa kuagiza vitu mbalimbali kwa njia ya msamaha wa kodi huku wakifanya biashara ya vitu hivyo kinyume na makusudio ya msamaha waliomba na kupewana serikali”, alisema na kuongeza.



“Jambo hili lilishawahi kuthibitishwa na serikali ya awamu ya nne kupitia Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alipobaini uwepo wa magali yaliyoingia kwa njia ya msamaha wa kodi na kukutwa yadi yakiuzwa kama mali ya kibiashara ya mtu binafsi mpaka serikali ya awamu ya nne ikafikiria namna ya kuondoa swala la msamaha wa kodi kwa taasisi za Dini ili kulinusuru Taifa na ufisadi wa kimazingira kupitia baadhi ya taasisi za Dini”.



Aidha ‘Bush Lawyer’ amesema TEC ni vema ikajipambanua kuwa wanapinga mkataba wa bandari kutokana na maslahi yao binafsi badala ya kujiegemeza na kudai ni sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ilihali hawakutuambia utafiti wa kujua watu wengi hawakubaliani na mkataba huo waliufanya kwa kutumia sampo gani.



Kuhusu haki ya kutoa maoni na kujieleza, Bush lawyer alisema kuwa, kila Mtanzania yuko huru kutoa maoni yake juu ya suala lolote lile kwa lengo la kujenga na kustawisha maendeleo ya Taifa letu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 18. kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (1-2).



Hata hivyo amesema kwa kuzingatia ibara ya 26 kifungu kidogo cha kwanza na chapili (1-2) maoni sio kejeri, dharau, uwongo, uzushi, kashfa, matusi au kupinga uwamuzi wowote wa kisheria bila kufuata taratibu za kisheria zinazotajwa ibara ya 30 kipengele kidogo cha (3) na cha (5). Hayo sio maoni yanayotakiwa na ibara hizo tajwa hapo juu na vipengele vyake ispokuwa ni uwasi na uvunjifu wa katiba ya nchi katika kuathiri utekelezaji wa mamlaka za nchi na sheria zake.



Katika hatua nyingine ‘Bush lawyer ameishauri serikali kuangalia upya juu ya uwezekano wa kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa yenye dhamira ovu ya kuvunja umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.



“Kutokana na sababu za kiusalama tunaishauri serikali isitishe kwa dharura mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ambavyo vinaonekana vikitumia mikutano hiyo kukejeri, kudharau, kukashifu, kutukana viongozi wa serikali na mamlaka zake pamoja na kuchochea wananchi kutokuwa na Imani na mahusiano mazuri na Serikali yao.



‘Bush Lawyer’ amesema ushauri huu ni umuhimu ukazingatiwa kwa dharura na kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi kwa sababu katika utendaji wa shughuli za kisiasa uko muda wa kufungua kampeni na upo mwisho wa muda wakufunga kampeni hivyo hakukuwa na sababu yoyote ya kimaendeleo na uchumi wa Taifa kuruhusu harakati ya kufanya mikutano ya kisiasa kwa vyama ambavyo vimeshindwa kupata ridhaa ya wananchi.

No comments:

Post a Comment