Tuesday, August 22, 2023

BILIONI 19.5 KUTUMIKA KUBORESHA BANDARI YA BUKOBA.




 Na Alodia Babara- Bukoba. 

Bandari ya Bukoba inatarajia kutumia Sh19.5 bilioni kwa ajili ya kuiboresha na kuipanua kwa kujenga gati mpya, kuboresha magati yaliyokuwepo, ujenzi wa jengo la abiria na ujenzi wa maegesho ya magari.


Mkuu wa Bandari ya Bukoba Michael Palangyo akizungumza na waandishi wa habari jana Agosti 21,2023 amesema kuwa ujenzi huo umeanza toka Februari, 2023 ujenzi utakuwa wa mwaka mmoja na nusu hadi sasa ni miezi sita.


Alisema tayari mkandarasi ameishafanya kazi takribani asilimia 13, na ujenzi utakamilika Julai 2024 ma utagharimu Sh19.5 bilioni hadi kukamilika kwake.


"Ujenzi huu umeanza toka Februari, 2023 utachukua mwaka mmoja na nusu,  hadi sasa ni miezi sita, mkandarasi ameishafanya kazi takribani asilimia 13 na ujenzi utakamilika Julai 2024 hadi kukamilika kwake utagharimu Sh19.5 bilioni" amesema Palangyo 


Palangyo amesema, upanuzi na uboreshaji wa Bandari unahusisha ujenzi wa gati jipya na kuboresha yaliyopo, ujenzi wa jengo la abiria, ujenzi wa miundombinu ya umeme na maji ya mvua na maegesho ya magari.


Ameeleza kwamba, ujenzi wa Bandari hiyo si tu ni kwa ajili ya kupokea meli kubwa ya Mv Mwanza hapa kazi tu bali ni sehemu ya kuboresha mazingira kwani yamebadilika.


Aliongeza kwa kusema kuwa, toka ilipojengwa Bandari hiyo mwaka 1945 kumekuwa na maboresho madogo madogo lakini kwa sasa hayo ni maboresho makubwa na ni sehemu ya kuboresha huduma kwa wananchi.


Aidha wajumbe wa bodi ya Wakala wa huduma za meli TASAC wametembelea Bandari ya Bukoba, Kemondo na kiwanda cha kuchakata minofu ya sangara kilichopo Bukoba, huku mjumbe wa bodi hiyo King Chiragi akieleza lengo la ziara hiyo kuwa ni kubaini changamoto zinazokabili usafiri wa majini na kuzitafutia ufumbuzi na mwisho wa siku usafiri wa majini uwe salama na Bandari na mialo zifanye kazi zao kwa ufanisi.


Mmoja wa wananchi Adelina Kubalyenda amesena uboreshaji wa Bandari hiyo utasaidia abiria kupata jengo la kupumzika na kuondoa changamoto hiyo na upanuzi utasaidia kuwepo mzunguko wa fedha baada ya kuongezeka meli na vyombo vingine vya majini.




Pichani ni shughuli za ukarabati na upanuzi wa Bandari ya Bukoba zikiendelea.


No comments:

Post a Comment