Akiongea kwenye mkutano mkuu wa Bakwata mkoa wa Arusha hibi karibuni, Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Jabir Mruma, amesema sasa kuna haja kubwa kuweka utaratibu mzuri na wa wazi kuwawezesha masheikh wanaofanya kazi ya dini kwenye ngazi zote Madrasa, Misikitini NK. walipwe mishahara minono ili wawe na pato halali kwa kazi wanazofanya badala ya kuwaacha na kuwawekea mazingira ya kuwalaumu au kwadhania kuwa wanajipatia pato kwa njia nyingine.
Amesema kwa kuwa muda wao wote ni kuwahudumia waislamu ni muhimu waislamu wawaandalie mazingira mazuri na ya wazi kuwawezesha kupata pato ili waendelee kuwahudumia waislamu huku wakiendesha maisha yao na familia zao kama wafanyakazi au wanajamii wengine.
Wakati huohuo Katibu Mkuu huyo wa BAKWATA aliongeza kwa kusema kuwa viongozi wa BAKWATA wanapaswa kujenga utamaduni wa kuambizana ukweli pale ambapo mmoja amekosea ili kujenga nidhamu ya maadili na uadilifu katika uongozi.
"Ili tufanikiwe lazima sisi viongozi wa Bakwata tujenge utamaduni wa kuambizana ukweli, mmoja wetu akienda kombo au akijisahau tuna wajibu wa kumwambia, tutamsaidia yeye, Baraza na waislamu kwa ujumla" Alisema.
"Tusinyamazie makosa kwa sababu tutaanguka sisi sote, muhimu ni kutumia lugha nzuri kuambizana na siyo kukashifiana au kutukanana, Alimalizia Sheikh Mruma.
No comments:
Post a Comment