Saturday, August 26, 2023

WADHIBITI UBORA WA SHULE NCHINI WATAKIWA KUZINGATIA VIWANGO VYA UBORA KATIKA ELIMU

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na Wathibiti ubora wa shule jijini Arusha.
...................................

Na.Mwandishi Wetu-ARUSHA

Wadhibiti Ubora wa Shule nchini wametakiwa kuhakikisha shule zinakuwa na viwango vilivyowekwa na Serikali katika miundombinu, ufundishaji, vitendea kazi na maudhui yanayofundishwa watoto ili kuwawezesha kupata elimu iliyo bora.

Akizungumza na Wathibiti ubora wa shule Jijini Arusha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa wazazi wanawapeleka watoto shuleni wakiwa na matumaini ya kwamba zina viwango vinavyotakiwa na wanafundishwa kwa kufuata maudhui yaliyowekwa ambayo yanalinda tamaduni za nchi.

“Naomba muangalie maudhui wanayofundishwa watoto, wazazi wanatuachia watoto wao tunakaa nao shule, matarajio yao ni kuona yale wanayosimamia nyumbani sisi tunaendelea kuyasimamia shuleni hivyo ni wajibu wenu kuangalia vitabu vilivyopo shuleni na maudhui yanayofundishwa” amesema Prof. Mkenda.

Waziri huyo ameongeza kuwa ni wajibu wa Wadhibiti ubora kutoa taarifa kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa juu ya changamoto wanazokutana nazo za miundombinu na upungufu wa walimu wanapofanya ukaguzi na kufatilia kwa karibu ili zipatiwe ufumbuzi badala ya kukaa kimiya na kungoja zianze kusambaa katika mitandao ya kijamii.

“ Maeneo ambayo ningependa muyawekee macho ya ukaribu ni changamoto ya vyoo vya wanafunzi na walimu , ninajua kuwa halmashauri hazishindwi kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, hivyo hatupaswi kuwa na shule zisizokuwa na vyoo ama zenye vyoo vibovu, nasisitiza katika hili embu geukeni kuwa wanaharakati” amesisitiza Waziri huyo.

Aidha, Prof . Mkenda amesema baada ya muundo wa udhibiti ubora wa shule kubadilika wadhibiti hao wamepewa rungu la kusimamia na kufuatilia viwango na pale mambo yasipotekelezwa wanaweza kuchukua hatua lakini amewataka wadhibiti hao kuona namna ya kusaidia katika kutatua changamoto na kuwezesha kutatua chamgamoto zinazokutwa shuleni.

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Shule, Simbeye amesema malengo ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na uelewa Wadhibiti Ubora wa Shule kwenye maeneo ya utekelezaji wa Mradi wa SEQUIP, Programu ya Shule Salama kwa Shule za Msingi na Sekondari na kuwapa mbinu za kukagua utekelezaji wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini.

Ameongeza kuwa pia Wadhibiti hao watapitishwa kwenye Muundo Mpya wa Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ambao umeondoa ofisi za Kanda na kubaki na za Mikoa, Wilaya na Shule pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuongeza idadi ya asasi za kufanyiwa tathimini kutoka kwenye lengo la asasi 8000 hadi kufikia 10,000.

Naye Mratibu Msaidizi wa Mradi wa  Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Beatrice Mbigiri amesema mafunzo hayo yamejumlisha Wakufunzi wapatao 215 na kwamba kupitia mafunzo hayo utekelezaji na uendeshaji wa elimu ya Sekondari utakuwa wa mafanikio.



Mkurugenzi Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule Bw.Ephraim Simbeyi,akizungumza wakati  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na Wathibiti ubora wa shule jijini Arusha.


Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati akizungumza na Wadhibiti ubora wa shule jijini Arusha.


No comments:

Post a Comment