Saturday, August 5, 2023

NAIBU WAZIRI: IJA NI CHUO MUHIMU KWENYE MAMBO YA HAKI.

 

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ni Chuo muhimu katika kuwajenga watu wanaosimamia masuala ya haki hapa nchini.


Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amesema hayo leo Jumamosi tarehe 05/08/2023 wakati akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya IJA, Halmashauri Tendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU) tawi la Lushoto pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, hapa Chuoni wilayani Lushoto.


Amesema kuwa Chuo cha IJA kinapotoa maarifa kwa watu wa kada mbalimbali, basi kinasaidia katika masuala ya haki, akibainisha kuwa wananchi mbalimbali bado wanakabiliwa na ukosefu wa haki.


"IJA ni Chuo muhimu, nimefurahi kuona kumbe tuna Taasisi nzuri hapa," amesema Naibu Waziri na kuongeza,
"Sisi ambao tuna husika na wananchi moja kwa moja kama wabunge, madiwani na wenyeviti ni mashahidi kwamba wananchi wetu bado wana ukosefu wa haki zao hasa masuala ya kisheria, kwa hiyo nina imani ninyi mkiwapa maarifa watu wanaokuja kusoma hapa mnakuwa mnasaidia kwenye eneo la haki."


Pia Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria ameongeza kuwa amejifunza masuala mengi ya Chuo cha IJA na kuhusu changamoto za Chuo Cha IJA, amebainisha kuwa atakwenda kuzifanyia kazi pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria na viongozi wengine.


"Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria alikuja hapa akapokea changamoto zenu, nami niwaambie tutakwenda kuzifanyia kazi na kazi yetu sisi ni kuwa kiungo ili kuona mnafanya kazi vizuri," amebainisha Mhe. Naibu Waziri.


Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha IJA ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F.Kihwelo amesema kuwa Chuo ni kitovu cha elimu na Utafiti kwa upande wa Mahakama na kwamba kimeendelea kuzalisha watu muhimu kwenye eneo la usimamizi wa haki.


Pia Mhe. Jaji Kihwelo amesema kuwa Chuo kimefarijika na ujio wa Naibu Waziri hapa Chuoni na kwamba ziara hiyo imekuwa na tija.


Awali katika ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria alitembelea maeneo kadhaa ya Chuo, ikiwemo Maktaba, Hosteli ya Wanaume ya Benjamini Mkapa pamoja na viwanja vya michezo vya Chuo.





No comments:

Post a Comment