Wednesday, August 16, 2023

DC. BAGAMOYO AHIMIZA WATENDAJI KUIMARISHA UTALII.

 


Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya ushauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Halima Okash, amewaagiza Watendaji wa Idara na taasisi mbalimbali zilizopo kwenye wilaya hiyo kuweka mkazo kwenye suala la utalii ndani ya wilaya hiyo.


Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya kilichofanyika leo tarehe 16 Agosti 2023 katika ukumbi wa Halmshauri ya Wilaya ya Bagamoyo na kuwahusisha Wenyeviti, Wakurugenzi na Watumishi wa idara mbalimbali katika halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze, Bi. Halima amewataka wajumbe wa kikao hicho kuwa mabalozi wa utalii katika idara zao na taasisi wanazotoka.


"Hili ni agizo nawaomba wakuu wa idara kuandaa utaratibu kwa watumishi waliopo kwenye idara zenu kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika halmshauri zetu" ameagiza, Bi. Halima.


Amewasisitiza maafisa elimu kuhakikisha kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanatembelea na kuvielewa vivutio mbalimbali vya utalii vilivyomo katika wilaya ya Bagamoyo.


"Niwaombe Maafisa Elimu kuandaa utaratibu mzuri kwa wanafunzi wa shule zetu zilizopo wilaya ya Bagamoyo kutembelea vivutio vyetu vya utalii kwa kufanya hivyo tutaongeza ufahamu na kuvitangaza kirahisi hivyo kuwa na ongezeko la watalii litakalopelekea kukua kwa mapato kupitia sekta hii" aliongeza Bi. Halima.


Wilaya ya Bagamoyo imekuwa na vivutio mbalimbali vya utalii kama vile Mbunga ya Saadan ambayo ni mbuga pekee nchini inayopakana na fukwe za bahari, mji mkongwe wa kaole, fukwe tulivu zenye mandhari ya kuvutia za bahari ya hindi, na soko la watumwa.


Aidha Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati mbalimbali ya kukuza utalii hapa nchini kwakua utalii ni sekta inayoingiza fedha nyingi zinazosaidia kujengwa kwa miradi mbalimbali kwenye jamii.






No comments:

Post a Comment