Wednesday, August 16, 2023

TFS YAPANDISHA HADHI MISITU 15 KUWA HIFADHI YA TAIFA KUTUMIKA KWENYE UTALII NA UWEKEZAJI

 


Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS), Prof.Dos Santos Silayo, akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari leo Agosti 16,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo na Mwelekeo wa utekelezaji  kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

...................

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAKALA wa Misitu Tanzania( TFS ) umefanikiwa kupandisha hadhi Misitu ya hifadhi 15 kuwa Misitu ya hifadhi ya Taifa na Misitu ya hifadhi za mazingira asilia mitano 5 yenye ukubwa wa hekta 58,216 katika kipindi Cha Mwaka 2022/2023 ambapo Upandishaji hadhi huo,utafanya Misitu hiyo kutumiwa kwa shughuli za utalii na uwekezaji.


Hayo yamesemwa leo Agosti 16,2023 jijini Dodoma na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS), Prof.Dos Santos Silayo,wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo na Mwelekeo wa utekelezaji  kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.


Prof. Dos Santos, ameitaja Misitu hiyo kuwa  ni; Kindoroko (Mwanga), Nou (Mbulu/Babati), Uvinza (Uvinza), East Matogoro (Songea) na Hassama Hill (Mbulu). 


Kamishna huyo ameeleza kuwa kufuatia juhudi za serikali ikiwemo ubunifu wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuandaa filamu ya “Tanzania the Royal Tour” ambayo imeitangaza Tanzania  ndani na nje ya nchi kwa kiasi kikubwa, TFS imejipanga kutumia fursa hiyo kuongeza tija katika uhifadhi, utalii na ukusanyaji maduhuli.


“Juhudi  hizo zimesaidia  kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia ambapo hadi kufikia Juni 2023 jumla ya watalii 242,824 walitembelea vivutio hivyo,”alisema


“Idadi hii ni ongezeko la asilimia 60.8 ukilinganisha na watalii 152,002 waliotembelea vivutio hivyo kwa kipindi hicho kwa mwaka 2021. Jumla ya sh.bilioni  1.3  zilikusanywa ikilinganishwa na sh.milioni 603.3 zilizokusanywa mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la Asilimia 126.9.”


Amebainisha  kuwa :”Katika kipindi cha miaka miwili TFS imeanzisha shamba jipya moja la Makere Kasulu-Kigoma, na kufanya upanuzi wa mashamba mawili,


Katika hatua nyingine, profesa Silayo amesema katika mwaka wa fedha uliopita, TFS ilizalisha jumla ya tani 25.9 za mbegu za miti na kuotesha miche  milioni 32.7 ya aina mbalimbali ambayo ilipandwa katika mashamba 24 ya serikali na mingine kugawiwa kwa watu binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kupandwa katika maeneo yao.

Amesema  kuwa hadi sasa, TFS imepanda miti katika hekta 6,909 na kurudishia miti iliyokufa kwenye hekta 2,434 pamoja na kuendeleza mashamba ya miti kwa kupalilia hekta 31,197, kupogolea hekta 8,353 na kupunguzia miti kwenye hekta 2,785.

”Wakala umeandaa mkakati wa usimamizi na uendelezaji wa mashamba ya miti ya serikali wa miaka 30 kuanzia 2021 – 2050  ambao umelenga kupanua wigo wa aina ya miti ikiwemo ile ya madawa kama vile Prunus africana na mpira . 


Miti hii imeanza kupandwa katika mashamba ya Mbizi, Wino, Rongai, Saohill, Iyondo Mswima, Meru na Shume,”ameeleza




No comments:

Post a Comment