Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo kutoka Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Fredrick Shoo ikiwa ni kwa ajili ya jitihada zake za kuleta Maendeleo nchini wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa hilo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Mfuko wa Wastaafu Mkoani Arusha tarehe 21 Agosti, 2023
..........................
Jumatatu tarehe 21 Agosti 2023
Miongoni mwa mambo yaliyosubiriwa kwa hamu kubwa katika siku ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) ni hotuba ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo.
Hotuba ya Baba Askofu Shoo ilijaa hekima, maarifa na falsafa kubwa kiasi kwamba ilihitaji utulivu wa hali ya juu kuweza kumuelewa.
Baba Askofu alisema na hapa ninamnukuu:
"Lipo hili la DP World Mheshimiwa. Kwanza naomba tu ieleweke wazi kwamba kanisa linaunga mkono uwekezaji. Hatupingi uwekezaji Mheshimiwa Rais, na tunajua, wewe, kwenye nia yako unataka wawekezaji.
Hata hivyo, jambo hili limekuwa na maoni mbalimbali ya wananchi na vyombo vya habari, viongozi wa dini zote, kwenye vyombo vya habari, kwenye mitandao n.k tumeona maoni mbalimbali.
Lakini Mheshimiwa Rais unatambua kwamba sisi viongozi wa dini zote, kwa uwakilishi, tuliomba kuja kukuona. Pale mwanzoni kabisa mwa jambo hili, na kwa uungwana wako, na kwa unyenyekevu ulio nao, utayari wa kusikiliza, Mheshimiwa Rais ulitupokea na tulikuletea maoni yetu kama taasisi na viongozi wakuu wa dini katika nchi yetu ya Tanzania.
Madhehebu yote ya kikristo, tukiwa CCT, tukiwa TEC, tukiwa Bakwata.
Mimi nakumbuka jinsi ulivyotupokea, ukatusikiliza, ukapokea maoni yetu na ushauri wetu viongozi wa dini na ukaahidi kuwa maoni na ushauri huo utayapeleka kwa wataalamu na kufanyiwa kazi kwa uzito unaostahili kwa maslahi mapana ya taifa.
Tuna imani na wewe Mheshimiwa Rais. Tunakuamini Mheshimiwa Rais na tunaamini kwamba ukisema, taasisi zako na vyombo vyako vitafanyia kazi jambo hili, unamaanisha hivyo.
Sasa najua, katika jambo hili tunaelekea mahali ambapo tunataka kugawanyika kabisa, na wengine wanatumia sababu za kidini, wengine maslahi yao ya kisiasa, na wengine kiuchumi.
Tunashukuru Mungu amekujaalia hekima katika hili, kama mama na kiongozi, umekaa kimya. Na kimya chako hiki Mheshimiwa Rais siyo kwamba hulifanyii kazi.
Mimi nasema jambo hili linahitaji hekima kubwa ya kuliendea na sisi kama tulivyosema tunaendelea kukuombea kwa Mungu ili hekima yote itumike katika kuweza kuleta muafaka wa jambo hili pasipo kuwagawanya au wananchi kugawanyika na kutumika kama kitu cha kuchochea wananchi kwa watu wenye malengo yao mengine. Mheshimiwa Rais, kanisa liko pamoja nawe." Mwisho wa kunukuu.
Baada ya kumaliza kusoma hotuba yake Askofu Mkuu Dkt. Fredrick Shoo alimkaribisha Mgeni Rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhutubia wahudhuriaji.
Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais alisema na hapa ninamnukuu:
"Ndugu zangu na hasa kaka yangu, Baba Askofu Shoo, nimeyasikia yote uliyosema kuhusu usalama, amani, umoja na muendelezo wa taifa letu.
Niliamua kunyamaza kimya na naendelea kunyamaza kimya.
Ninachotaka kuwahakikishia, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa taifa hili.
Hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuuza taifa hili.
Hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye taifa hili.
Sasa hayo itoshe kuwa ni ujumbe wangu kwenu. Asanteni sana!" Mwisho wa kunukuu.
Hotuba hizi mbili, ile ya kwanza ya Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Fredrick Shoo na ile ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan zinabainishia mambo yafuatayo:
(i) Kwamba, KKKT inaunga mkono uwekezaji ukiwemo wa DP World. Lakini ni muhimu kwa serikali kuzingatia ushauri na maoni yanayotolewa na wadau mbalimbali juu ya uendeshaji wa bandari hiyo.
(ii) Kwamba, viongozi wa madhehebu yote ya dini nchini walikwenda Ikulu na kukutana na Mheshimiwa Rais na kutoa maoni na ushauri wao juu ya uendeshaji wa bandari na serikali ikayapokea na kuwaeleza viongozi hao kuwa yatafanyiwa kazi.
(iii) Kwamba, Mheshimiwa Rais ameyapokea maoni na ushauri uliotolewa na viongozi wa dini na amewapa wataalamu kuchakata maoni na ushauri huo ndiyo maana amekaa kimya akisubiri wataalamu wamalize wampe mapendekezo awaite viongozi wa dini awape mrejesho.
(iv) Kwamba, wapo watu wanaotumia suala la DP World kwa mrengo wa kidini, wengine wakitumia hilo kama kete ya kisiasa ya kupata uungwaji mkono na wengine kujiunufaisha kiuchumi pasina kujali athari zinazoweza kutokea kwenye nchi.
(v) Kwamba, wapo watu wanaotumia suala la DP World, si kwa maslahi ya taifa bali kwa lengo la kuvuruga amani na kuleta machafuko nchini ndiyo maana Mheshimiwa Rais alionya kwamba, hakuna mwenye ubavu wa kuligawa taifa wala kuharibu amani na usalama uliopo au kuliuza taifa kwa gharama yoyote ile.
Aidha, hotuba hizi mbili, ya Askofu Shoo na ya Mheshimiwa Rais Samia zinatupa maswali kadhaa ya kujiuliza kutokana na Tamko la TEC lililotolewa Ijumaa Agosti 18 2023.
(a) Kama viongozi wa TEC walikuwa miongoni mwa viongozi wa dini walioenda Ikulu kutoa maoni na ushauri, kwa nini wasingesubiri kuona kama maoni na ushauri wao umefanyiwa kazi au lah kabla ya kutoa Tamko?
(b) Kama TEC waliamua kutoa Tamko, ina maana kuwa hawamuamini Mheshimiwa Rais kuwa atafanyia kazi maoni na ushauri waliotoa? Tukumbuke Baba Askofu Dkt. Shoo yeye alisisitiza kuwa KKKT lina imani na Rais hivyo wanaamini atayafanyia kazi maoni na ushauri waliotoa, vipi kwa TEC?
(c) Tamko la TEC lilieleza kwamba TEC imefuatilia kwa umakini mijadala, maoni, mapendekezo na vilio vya wananchi walio wengi ambao ni wamiliki wa bandari na rasilimali zote na wametambua kuwa wananchi walio wengi hawautaki Mkataba wa DP World, je maoni waliyotoa kwa Rais hayakuwa na tija?
(d) Kwa nini TEC hawakukutana na viongozi wenzao wa dini kama awali na kuwaeleza kubadilika kwa msimamo wao kama ambavyo walikutana hapo awali na kwenda kwa Rais kutoa maoni na ushauri wao?
(e) Tamko la TEC limeweka msimamo kuwa wao hawaungi mkono Mkataba wa DP World ilhali KKKT wameweka wazi kuwa wanaunga mkono uwekezaji ukiwemo wa DP World kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa dini. Je, itakuwaje kama Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na viongozi hao wakiwemo wa TEC na makubaliano kuendelea hatua nyingine?
Mtazamo wangu usio na tija:
Suala si bandari, suala ni uchaguzi wa 2025.
Dini zinatumiwa kama mwamvuli na baadhi ya wanasiasa kutafutia huruma (appealing to sympathy/pity).
Nyoka aliye ndani ya nyumba anahitaji hekima kubwa kama aliyosema Baba Askofu Dkt. Shoo kumtoa la sivyo utavunja vyombo na kupata hasara au atakugonga au kukurushia mate ya sumu.
Kuna nyoka pahala. Lipo tatizo pahala. Umakini , weledi na hekima vinahitajika.
Asanteni:
Wenu:
No comments:
Post a Comment