Thursday, August 17, 2023

MKUU WA CHUO IJA AWATAKA MAHAKIMU WAKAZI WAPYA KUWA WANYENYEKEVU


 Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewataka Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za mwanzo kuwa wanyenyekevu ili iwasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Kihwelo ameyasema hayo alipozungumza na Wahe. Mahakimu hao wanaoendelea kupatiwa Mafunzo Elekezi ya siku tano hapa IJA Lushoto mkoani Tanga.

Katika nasaha zake, Mhe. Jaji Kihwelo amesema: " Ushauri wangu kwenu nyote, be humble (kuweni wanyenyekevu), hii itawasaidia sana katika maisha yenu, msiwe watu wa kujikweza sana."


Vilevile, Mhe. Kihwelo amewataka Mahakimu hao kufanya kazi kwa kushirikiana miongoni mwao pamoja na Taasisi zingine zikiwemo za Serikali katika namna ambayo haitaathiri majukumu yao.


Kwa upande mwingine, Mhe. Dkt. Kihwelo amewashauri Mahakimu hao kila mmoja kumtegemea Mwenyezi Mungu kulingana na imani yake ili imsaidie katika utoaji wa maamuzi.


Aidha Mhe. Dkt Kihwelo ametoa wito kwa washiriki hao kujitahidi kusoma sana kwa minajili ya kujiongezea maarifa huku akibainisha kuwa maarifa ni nguvu.


Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA),


yalifunguliwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma mnamo Agosti 14, 2023 na yatamalizika Agosti 18, 2023

No comments:

Post a Comment