Jumla ya vijana 70 wasiokuwa na uwezo wa kutoa mahari wamefungishwa ndoa kwa pamoja jijini Dar es Salaam kwa msaada wa Taasisi ya Al hikma Foundation.
Ndoa hizo zimefungwa kwenye ukumbi wa DYCCC, Chang'ombe na kushuhudiwa na maelfu ya watu pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Spika wa bunge la Tanzania, Mussa Azan Zungu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally
Mkurugenzi wa Taasisi iliyoratibu ndoa hizo, Al Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki amesema kilichowasukuma kuwasaidia vijana hao kwa kuwatolea mahali ni kutokana na gharama za ndoa kuwa juu kulinganisha na uwezo wa maisha yao...
"Tulipokea ujumbe zaidi ya 1000 baada ya kutangaza jambo hili mwezi wa nne, waliojaza fomu za kutaka kusaidiwa kuoa walikua zaidi ya 200 lakini baada ya usaili tumepata 70 ambao leo wameoa", alisema Kishki.
Moja ya vigezo muhimu vilivyotumika kuwapata vijana hao ni nia yao ya kuoa, uwezo wa kumudu ndoa na wale ambao hawaongezi mke wa pili.
Mbali na kupewa nasaha za uvumilivu kwenye ndoa kutoka kwa viongozi karibu wote walioshiriki, mmoja wa vijana aliyeoa leo, Ally Ismail Mwaluka, mlemavu pekee katika kundi la waliooa anasema ni ndoto iliyotimia.
"Sikutarajia, wakati mwaka unaanza sikua hata na ndoto ya kuoa, leo nmeoa bure na nimepata vitu vingine juu kutoka kwa viongozi wa serikali, bajaji, mafuta ya bajaji kwa mwaka mzima na fedha mbalimbali, sina cha kusema namshukuru Mungu", alisema Ally.
Vijana hao wametoka mikoa 12 ya Tanzania bara na Visiwani na mahari waliozosaidia zimegharimu shilingi zaidi ya milioni 70 za kitanzania.
No comments:
Post a Comment