Friday, August 18, 2023

JAJI NONGWA AWATAKA MAHAKIMU WAKAZI WAPYA KUFANYA KAZI KWA UFANISI.

 


Jaji wa Mahakama Kuu, kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa amewataka Wahe. Mahakimu wakazi wapya wa Mahakama za mwanzo kufanya kazi kwa uweledi, uadilifu na uwajibikaji bila kujali kuwa wao bado ni wageni katika kazi hiyo mpya.

Mhe. Nongwa ametoa kauli hiyo leo Agosti 18, 2023 wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya siku tano kwa Mahakimu wakazi wapya wa Mahakama za mwanzo, yaliyokuwa yanafanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Mafunzo hayo ambayo yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na IJA, yalifunguliwa Agosti 14, 2023 na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma.

Mhe. Nongwa amewaambia Mahakimu hao:"Huna budi kufanya kazi kwa ufanisi na ubora mara tu unapotoka hapa, maana wewe ni Hakimu halisi sio mwanafunzi tena."

Pia amewakumbusha watambue kwamba majalada ya mashauri wanayokwenda kuyashughulikia ni maisha halisi ya mtu na hivyo wanapaswa kuwa makini na uamuzi wao watakaokuwa wanautoa.

Kwa upande mwingine, Mhe. Nongwa amewashauri Mahakimu hao kuzingatia maadili kwa kujiepusha na rushwa kwa kuwa rushwa ni adui wa haki.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Hakimu Mkazi mpya Mhe. Dina Mgoloka ametoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake akiweka wazi kuwa mafunzo hayo yamewapa uamsho wa kufanya kazi.

"Kwa kweli mafunzo haya yote yameweza kuleta uamsho au morali kwetu sisi ya kufanya kazi, nasi tunaahidi kuyabeba kama nyenzo za kutuwezesha kufanya kazi za uhakimu kwa uadilifu, uweledi na uwajibikaji," amesema Mhe. Mgoloka.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu ameishukuru IJA kwa kuendesha mafunzo hayo kwa ufanisi pamoja na kuwashukuru Mahakimu hao kwa utulivu wao wakati wote wa mafunzo.









No comments:

Post a Comment