Thursday, August 24, 2023

WAZIRI MCHENGERWA AAGA KUNDI LA 19 LA WANANCHI WA NGORONGORO WANAOHAMA KWA HIARI.

 

Na Kassim Nyaki, NCAA.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa leo tarehe 24 Agosti, 2023 amewaaga rasmi wananchi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambao ni awamu ya pili ya waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda maoneo mbalimbali nje ya Hifadhi.

Kundi hilo la Wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro lililoagwa leo linajumuisha kaya 16 na zenye wananchi 87 na mifugo 740 ambapo kati ya kaya hizo, kaya 14 zinahamia katika maeneo ya Wilaya za Monduli, Karatu na Arusha ziliko Mkoa wa Arusha na kaya 2 zinahamia Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga.

Akiaga kundi hilo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa ameeleza kuwa Serikali katika awamu ya pili ya utekelezaji wa zoezi hili linaenda sambamba na ujenzi wa nyumba 5,000 za makazi katika maeneo ya Serikali yaliyopo Msomera Wilayani Handeni na eneo la Kitwai lililopo Wilaya ya Kilindi.

Ameongeza kuwa katika awamu hii ya pili ya utekelezaji wa zoezi Serikali imewapa uhuru wananchi kuhamia katika maeneo yaliyoandaliwa na serikali au maeneo yoyote ambayo mwananchi atachagua mwenyewe na serikali itakuwa tayari kuwapa stahiki zao kwa mujibu wa sheria na kusafirisha mali zao ikiwemo samani na mifugo.

Akitoa taarifa kuhusu wanaohama Naibu kaamishna wa Uhifadhi NCAA Elibariki Bajuta ameainisha kuwa katika awamu ya kwanza iliyoishia mwezi Januari 2023 jumla ya kaya 547 zenye watu 3,010 na mifugo 15,321 zilikwishahamia kwa hiari katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine kwa ajili ya kupisha shughuli za Uhifadhi.

Amebainisha kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 5000 unaoanza hivi karibuni utaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu ya kijamii ikiwepo barababara, vituo vya Afya, zahanati, maji, umeme, majosho, malambo na kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Mwl Raymond Mangwala ameeleza kuwa kwa sasa zoezi la uelimishaji, uandikishaji na uthaminishaji linaendelea na wale wote watakaohamishwa kwenda maeneo mbalimbali, Serikali itaendelea kuwalipa stahiki zao zote kwa mujibu wa sheria na kufuata misingi ya haki za binadamu.





No comments:

Post a Comment