Na Alodia Babara -ukoba.
Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa mwaka 2023/2024 inatarajia kupokea na kutumia shilingi bilioni 32 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato.
Kiasi hicho cha fedha kimetajwa jana na mwenyekiti wa kamati ya fedha na Utawala Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gybson wakati akisoma taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo.
Amesema, mwaka 2022/2023 Manispaa ya Bukoba ilipanga kuidhinishiwa na kutumia shilingi bilioni 32 wakatumia shilingi bilioni 28.4 sawa na asilimia 89.
"Kiasi hicho cha fedha ni kutoka katika vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo michango ya shule za sekondari, uchanguaji wa huduma za afya, ruzuku kutoka serikali kuu na wahisani wa maendeleo, hadi kufikia June 30,2023 Manispaa ilikusanya na kupokea shilingi bilioni 28.4 sawa na asilimia 89 ya makisio" amesema Gybson
Amesema kwa mwaka 2022/2023 makusanyo ya ndani walipanga kukusanya shilingi bilioni 3.5 zikakusanywa shilingi bilioni 3.2 sawa na asilimia 93.
Amesema halmashauri iliidhinishiwa kutekeleza miradi 52 ya maendeleo miradi 23 imekamilika, miradi 17 iko katika hatua za ukamilishaji na miradi 12 haijaanza kutekelezwa itatekelezwa katika kipindi cha robo ya kwanza mwaka 2023/2024.
Aidha diwani wa Kashai Ramadhan Kambuga amesema kamati ya fedha na Utawala wamebuni vyanzo vipya vya mapato ili Manispaa hiyo ipate fedha zaidi ya shilingi bilioni 3 ya sasa kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani.
Naye diwani wa kata ya Bilele Tawfiq Sharifu amesema kuwa, kiasi cha fedha shilingi milioni 5 kutoka mapato ya ndani zilizoidhinishwa na Baraza hilo kwa ajili ya kukarabati kila mwaka chumba kimoja cha darasa shule ya msingi Bilele ni kidogo kingeongezwa kutokana na uchakavu wa miundombinu ya shule hiyo ambayo ilijengwa tangu mwaka 1957.
Amesema, Manispaa ione umuhimu wa kuongeza kiasi cha fedha kwaajili ya kukarabati vyumba zaidi ya kimoja kwa mwaka kwani vyumba hivyo vinaweza kusababisha hatari kwa watoto wao kutokana na kuchakaa na hasa katika kipindi cha mvua za vuli ambazo kwa Kagera zimeanza kunyesha.
No comments:
Post a Comment