Jeshi la Polisi Mkoani Iringa kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama Barabarani ya Mkoa huo, wapo mbioni kuanza utekelezaji wa mpango kabambe wa kuweka camera za kisasa kwenye maeneo korofi kwenye barabara kuu inayounganisha Mkoa huo na Mikoa mingine na kwa kuanzia camera hizo zitafungwa eneo la Majinja Wilayani Mufindi na Mlima Kitonga Wilayani Kilolo ili kupunguza ajali za barabarani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Abri Asas @salimasas amesema hayo wakati kamati yake ikiongozwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ilipotembelea maeneo kadhaa ambayo ni korofi na yanayoongoza kwa kusababisha ajali nyingi Iringa.
Asas amesema uwekwaji wa camera hizo utasaidia kupunguza ajali barabarani kwasababu zitakuwa zinafanya saa 24 na zikifungwa Polisi katika Ofisi ya RPC, RTO na OCD watakuwa wanaona LIVE kila kinachoendelea Kitonga na kote zilikofungwa, pia amesema Madereva wakijua eneo lina camera watazingatia sheria za usalama barabarani.
Katika ziara hiyo ya siku mbili Kamati hiyo imetembelea Nyang’oro, Mlima Kitonga na eneo la Majinja ambalo lilipewa jina hilo kufuatia ajali ya barabarani iliyohusisha basi la Kampuni ya Majinja Express lililogongana na lori la mizigo na kusababisha vifo vya Watu 50 na wengine 23 kujeruhiwa March 11, 2015
No comments:
Post a Comment