Tuesday, August 22, 2023

BANDARI YETU NA USHAURI KWA RAIS SAMIA

 

Na Albert Kawogo.


SINA kumbukumbu na marais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi kwenye malalamiko kuhusu bandari lakini marais waliobaki hadi huyu wa sasa kwa nyakati tofauti wamelalamika juu ya ufanisi wa Mamlaka yetu ya Bandari na wao kuthibitisha kwa kauli ya ujumla kuwa Mamlaka hii ingekuwa inafanya kazi vizuri ingeweza kuchangia hata nusu ya mapato ya Bajeti yetu. Ni kweli kabisa naungana na Marais hawa kwenye hili.


Mfupa wa Bandari ni mfupa uliowasumbua Marais karibu wote waliowahi kutawala Tanzania! Hii imekuwa kawaida kila Rais mpya akiingia au Waziri Mkuu mpya akiteuliwa sehemu ya kwanza ni kwenda kulalamika na kuonya kuasa na hata kutumbua watendaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.


Kwa kumbukumbu zangu kuanzia kwa Mkapa, Kikwete, Magufuli hadi sasa Samia, Bandari hapajawai kupoa.


Hoja yangu kuu kwenye hili ni kwamba inawezekana sana bado hatujajua shida ni nini hasa pale Bandarini na kwa uelewa wangu mdogo napenda leo nimshauri Mhe Rais mambo ya kufanya na naamini kama nilivyoshauri kuhusu Ngorongoro na ikafanyika na sasa imefanikiwa basi nashauri juu ya hili la Bandari na naamini ikifanyika itafanikiwa


1. Lazima tukubali kuwa Bandari ya DSM haiwezi kuwa na ufanisi kwa sababu imekuwa finyu kuhimili idadi ya mizigo, Meli na Magari kiushindani


2. Lazima tukubali kuwa Serikali haiwezi kuendesha bandari kwa ufanisi tunaoutaka katika dunia hii ya ushindani. Bandari kubwa zote duniani na zinazofanya vizuri kwenye soko la ushindani kuanzia Dubai, Hong Kong, Singapore, New York na nyinginezo, zinaendeshwa either kwa sehemu kubwa na private sector au kwa ubia baina ya Serikali na sekta binafsi.


Hivyo ili kufanikiwa kupata ufanisi hapa Tanzania kwenye sekta ya Bandari , Lazima tutake tusitake, tufanye yafuatayo


a. Kwa haraka sana, Ijengwe Bandari ya Bagamoyo ambayo iwe na Gati zisizopungua 40. Bandari hii iendeshwe na Private sector with exception kwenye masuala ya Ulinzi, Usalama na Kodi


b. Sekta binafsi wapewe pia fursa ya kujenga Miundombinu ya Reli na barabara kuunganisha Bandari ya Bagamoyo na Jiji la Dar es Salaam ikiwemo reli ya kati SGR na TAZARA


c. Bandari za DSM, Tanga, Mwanza na Kigoma na Mtwara ziendeshwe kwa ubia na sekta binafsi. Serikali isimamie masuala ya kodi , ulinzi na usalama tu!


d. Barabara ya Mandela Road( DSM) itanuliwe kuwekwa njia 8 kutokea Bandarini hadi Ubungo na utanuzi wa njia 6 uendelee kutoka Kimara hadi Ubungo. Hii ni ili kuleta ufanisi wa usafirishaji mizigo katika Jiji la Dsm. Ikiwezekana sekta binafsi washirikishwe kwenye hili.


e. Kulikuwa na Mpango wa Kujenga Barabara ya Malori kutokea Bandarini hadi Chalinze. Mpango huu ufufuliwe na barabara hii ijengwe hata kwa kutumia sekta binafsi. Fedha zitarudi haraka sana hata kwa toll tax!


Nchi kubwa duniani ziliona hili na wakaamua kufanya! Hata kwa Tanzania Serikali iking'ang'ania kuendesha bandari kila siku mtaishia kushikana uchawi na kutumbuana!


Ni suala la kuamua tu na wakati ni sasa. 


No comments:

Post a Comment