Monday, August 14, 2023

MAHAKIMU WATAKIWA KUSHUGHULIKIA MRUNDIKANO WA MASHAURI.


Msajili mkuu wa Mahakama ya Tanzania afungua Mafunzo Elekezi ya Mahakimu Wakazi wapya 37, awataka kushughulikia mrundikano wa mashauri


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amefungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo leo tarehe 14/08/2023.


Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanafanyika hapa Chuoni IJA na yatadumu kwa siku tano hadi taehe 18/08/2023.


Katika hotuba yake ya Ufunguzi Mhe. Chuma ambaye alikuwa mgeni Rasmi, amewataka Mahakimu hao kwenda kusaidia kuondoa mrundikano wa mashauri katika Mahakama za mwanzo kama inavyotaka Sera ya Mahakama ya Tanzania. 


“Mpaka sasa bado Mahakama za Mwanzo zinaendelea kuongoza katika umalizaji wa Mashauri na kutokuwa na mrundikano wa mashauri, kwa hiyo tunategemea ongezeko lenu litaendelea kupunguza mzigo kazi wa kila hakimu na hatimaye kuendeleza sera ya Mahakama ya Tanzania inayotaka kutaka kusiwe na mashauri yanayozidi miezi sita,” amesema Mhe. Chuma.


Pia Mhe. Chuma amewataka mahakimu wakazi hao wapya kujifunza matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili waweze kutekeleza vema majukumu yao hasa wakati huu Mahakama ya Tanzania ikiwa imejielekeza katika eneo hilo la Teknolojia.


“Karne hii ya 21 imetawaliwa na matumizi ya Teknolojia katika kuwahudumia wananchi, jifunzeni matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayoendeshwa na Mahakama ili msipate ugumu mnapotekeleza majukumu yenu,” amesisitiza Mhe. Chuma.


Vile vile, Mhe. Chuma amewasisitiza washiriki hao kuwa wanapotekeleza majukumu yao, basi hawana budi kuzingatia misingi ya haki za binadamu, maisha ya watu na ustawi wa usalama wa nchi.


Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda amezungumzia umuhimu wa mafunzo hayo kwa kubainisha kwamba yanalenga kuwapatia Mahakimu hao miongozo itakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.


“Kimsingi umuhimu wa mafunzo haya ni kwa ajili ya kuwapatia muongozo Mahakimu wapya ambao wanaenda kuanza majukumu yao katika Mahakama za mwanzo, ukiwemo utoaji wa haki ambao ndio jukumu kubwa la Mahakimu hawa,” amesema Mhe. Dkt. Kisinda.








 

No comments:

Post a Comment