Wednesday, August 30, 2023

RAIS SAMIA YUKO SAHIHI KIKATIBA KUTEUA NAIBU WAZIRI MKUU


 Na Albert Kawogo


LEO hili Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri kwa kuteua Mawaziri wapya; kuwahamisha wengine; kuteua Manaibu Mawaziri na kuwahamisha wengine na kuwateua Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu na kuwahamisha wengine.


Kingine na kikubwa zaidi ni uteuzi alioufanya Mhe. Rais Samia kumteua Dkt. Doto Biteko kuwa Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Hili ni kubwa kwakuwa limeanzisha mjadala kwa wadau, wakiwemo wanazuoni mbalimbali kudai kuwa uteuzi huo (wa Naibu Waziri Mkuu) umekiuka Katiba.


Kikatiba, Mhe. Rais yuko sahihi. Ibara ya 36, Ibara Ndogo ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa Rais, pamoja na mambo mengine, kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inasomeka:


36.-(1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. 


(2) Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuziunaofanywa na Rais.


(3) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2), masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria yoyoteinayohusika, mamlaka ya kuwateua watu wengine wotewasiokuwa viongozi wala watendaji wakuu, kushika nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na pia mamalaka ya kuwapandisha vyeo watu hao, kuwaondoa katika madaraka, kuwafukuza kazi na mamlaka ya kudhibitinidhamu ya watu waliokabidhiwa madaraka, yatakuwa mikononi mwa Tume za Utumishi na mamlaka mengineyo yaliyotajwa na kupewa madaraka kuhusu nafasi za madaraka kwa mujibu wa Katiba hii au kwa mujibu wa sheria yoyote inayohusika. 


(4) Masharti ya ibara ndogo ya (2) na ya (3) hayatahesabiwa kuwa yanamzuia Rais kuchukua hatua za kudhibiti nidhamu ya watumishi na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.


Ni wazi kuwa kabla ya leo ( achilia mbali wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi), hakukuwa na nafasi ya Naibu Waziri Mkuu. Leo, akitumia mamlaka yake kikatiba, Mhe. Rais ameanzisha nafasi hiyo ya Naibu Waziri Mkuu. Ili nafasi hiyo ifanye kazi, akamteua Dkt. Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.


Kwa mamlaka hayo hayo, leo hii hii, Mhe. Rais amefuta iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kuanzisha Wizara mbili: Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi. Na uteuzi wa Mawaziri; Manaibu Mawaziri na Makatibu Wakuu ukafanyika. Yote haya yamefanyika kikatiba.


Kimsingi, Katiba yetu ya sasa inaruhusu kuanzishwa na/au kufutwa kwa nafasi yoyote ile ya kimadaraka. Wengi wetu tunajua, kwa kutumia Katiba hii hii, Rais Mstaafu Mwinyi aliwahi kumteua Hayati Augustine Lyatonga Mrema kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Ilitumika Katiba hii hii na Ibara hii hii iliyorekebishwa mwaka 1984 na mwaka 2000. 


No comments:

Post a Comment