Friday, August 11, 2023

SAFARI YA WACHIMBAJI NCHINI CHINA KULETA TIJA – DKT. KIRUSWA

Naibu Katibu Mkuu Ataka watumie ziara kujifunza


Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameutaka ujumbe wa wadau wa Sekta ya Madini wapatao 100 wakiwemo wachimbaji wadogo, wachimbaji wa Kati, Wafanyabiashara wa madini na watoa huduma migodini wanaotarajia kwenda nchini China kuhakikisha safari hiyo inaleta matunda kwa kuleta wawekezaji wengi na kupata vifaa vya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa madini nchini.


Wadau wengine, wanaoshiriki katika ziara hiyo ni wataalam wa madini kutoka taasisi za Wizara ya Madini, taasisi za Fedha ikiwemo Benki ya CRDB na wadau wengine muhimu.


Dkt. Kiruswa ameyasema hayo katika hafla fupi ya kuiaga timu hiyo Agosti 11, 2023 jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa, ubalozi wa China kwa kushirikiana na Kampuni ya Touchbroad ya nchi hiyo imeandaa ziara ya wachimbaji kutoka Tanzania ili kuwawezesha kukutana na wawekezaji wa Sekta ya Madini nchini China, kutembelea viwanda vya kutengeneza mitambo na vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini na kuwawezesha kupata uzoefu na wafanyabishara wa madini waliopo China na kupata teknolojia za uchimbaji na uchenjuaji.


"Niwaombe kila mmoja wenu akiwa China ahakikishe anatimiza malengo yake kadri anavyoweza ili ujuzi mtakaoupata uje kuwasaidia kuboresha biashara zenu na kuongeza tija,” amesema Dkt. Kiruswa.


Vile vile, amezipongeza taasisi za fedha kwa kuendelea kuwasaidia wachimbaji na wafanyabiashara katika kuhakikisha wanapata mikopo ya fedha kwa kuwa karibu na wafanyabiashara wa madini na amewataka kuangalia uwezekano wa kupunguza riba ili kupata wateja wengi na kuruhusu wachimbaji wadogo kupata mikopo yenye riba ndogo.


Kwa upande mwingine, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewataka wachimbaji hao kutumia ziara hiyo kujifunza na kupata uzoefu watakapotembelea viwanda vya kutengeneza mitambo na vifaa vya uchimbaji.


Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini nchini (FEMATA), John Bina amesema kuwa, ziara hiyo nchini China inakwenda kufungua milango ya nchi kuvutia wawekezaji wengi kuendelea kuja kwa kuwa nchi ina sera nzuri katika uwekezaji.


Viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Mbunge wa Viti Maalum Iringa Dkt. Rita Kabadi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venence Mwasse, Mjumbe wa Bodi ya STAMICO Lucas Seleli, mwakilishi wa benki ya CRDB pamoja na wataalam kutoka Wizara na taasisi zake katika safari inayolenga kukutana na wawekezaji wa Sekta ya Madini nchini China. 








 

No comments:

Post a Comment