Wauza Nje Madini ya Thamani ya Shilingi Trilioni 2.24
Katibu Mkuu Mahimbali Aunda Timu ya Wataalam 9 Kutathmini Biashara ya Madini Nje
Dodoma
Wafanyabiashara wa Madini wametakiwa kuhakikisha wanarejesha nchini fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya madini nje ya nchi ili zisaidie kuimarisha uchumi wa nchi.
Hayo yamebainishwa Agosti 16, 2023 jijini Dodoma na Waziri wa Madini Dkt.Doto Biteko wakati wa kikao chake na wafanyabiashara hao kutoka nchi nzima na kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi wa Wizara na Taasisi zake, Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Maafisa Madini Wakazi kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Ameongeza kwamba, Sekta ya madini nchini imetawaliwa na uwekezaji wa mitaji kutoka nje ya nchi ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 5.1 cha Sera ya madini kinasisitiza ustawi wa masuala ya kiuchumi ikiwemo ustawi wa huduma za benki nchini ili kuleta manufaa kwa Serikali na sekta binafsi.
Amesema kutokana na kifungu hicho, wizara ingependa kuona fedha za mauzo ya madini zinarejeshwa nchini kama Sheria inavyoelekeza kupitia mifumo ya kibenki na kwa kuzingatia sheria zote za nchi na kuongeza kwamba, hayo yote yanalenga kuboresha shughuli za madini nchini kutokana na umuhimu wa Sekta hiyo kiuchumi.
Pia, Dkt. Biteko ametumia jukwaa hilo kuwapongeza wafanyabiashara hao kwa mchango wao mkubwa ulioiwezesha Sekta ya Madini kuwa kinara katika kuliingizia taifa fedha za kigeni na kueleza kuwa, mwaka 2022 madini yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 3,395.3 yaliuzwa nje ya nchi sawa na asilimia 56 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi. ‘’ Mauzo hayo ni ongezeko la asilimia 9 ikilinganishwa na mauzo ya Dola za Marekani milioni 3,116.40 mwaka 2021,’’ amesema Biteko.
Vilevile, Dkt. Biteko ametambua mchango wa wafanyabiashara hao kupitia Masoko ya Madini na kusema, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/23 Julai 2022 hadi Juni 2023, waliweza kuuza madini nje ya nchi yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.24.
‘’Katika kipindi hicho, Serikali ilikusanya kiasi cha Shilingi bilioni 157.44 kama malipo ya mrabaha na ada ya ukaguzi, sawa na asilimia 25 ya mrabaha uliokusanywa kwa madini yote. Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa mchango wenu huo,’’ amesema Dkt. Biteko.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara wa madini kuuza madini yao nje ya nchi bila kurejesha fedha za mauzo kwenye benki za hapa nchini na kueleza kwamba, Mwaka wa Fedha wa 2022/23 wafanyabiashara wa madini kupitia kampuni zao walisafirisha nje ya nchi jumla ya madini yenye thamani ya Dola za Marekani 952,926,784.
Amefafanua kwamba, bado kiwango cha fedha za kigeni kinachoingia hakilingani na thamani ya madini yanayouzwa na kuwataka kutumia kikao hicho kujitathmini na kueleza wizara kuwa, inataka kuongeza mchango wa fedha za kigeni unaotokana na Sekta ya Madini.
‘’Wizara ya Madini imeandaa mpango mkakati wa kuongeza mauzo ya madini nje ya nchi. Mpango huo utahakikisha kuwa Sekta ya Madini inaendelea kuwa ni miongoni mwa Sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika kuingiza fedha za kigeni nchini. Tunataka mlete fedha za kigeni, hakuna mtu atakayechukua hela yako tunachotaka Sekta ya Madini iwezeshe kununua bidhaa nyingine muhimu, tupate fedha za kigeni za kutosha kukuza uchumi wetu,’’ amesisitiza Biteko.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema kikao hicho kimelenga kujadili mwenendo mzima wa biashara ya madini.
Vilevile, amesema Wizara imepunguza idadi ya leseni za wafanyabiashara wa madini kutoka 700 hadi 150 ili kubaki na wafanyabiashara wachache wanaokidhi vigezo.
Aidha, akihitimisha kikao hicho, Katibu Mkuu ameitaja timu ya wataalamu 9 kutoka upande wa Serikali ikiwemo Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Wizara ya Fedha, Benki Kuu Tanzania, na Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) kwa ajili ya kutathmini mwenendo wa biashara ya madini nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu wa TAMIDA Leopold Kimaro ameishauri Serikali kuangalia masuala mbalimbali ikiwemo utoaji leseni kwa wafanyabiashara wa madini na kuongeza kwamba, chama hicho kiko tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha suala hilo la mwenendo wa biashara ya madini yanayouzwa nchi ya nchi linafanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment