Thursday, August 24, 2023

WAISLAMU MORO WALIA NA MKURUGENZI WA MANISPAA KUWANYANG’ANYA ENEO WALILOPEWA KUJENGA MSIKITI

 


Na Rashid Mtagaluka

Wakazi wa mtaa wa Mjimwema ‘B’ kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro wamemuomba Mkuu wa mkoa wa Morogoro Alhaj Adam Kighoma Malima kuingilia kati suala la eneo la wazi lililopo mtaani humo ambalo awali lilitolewa kwa Waislamu wa mtaa huo kujenga msikiti kabla hakujazuka tafrani.

Maombi hayo wameyatoa Jumapili wiki iliyopita mjini Morogoro wakati wakizindua rasmi ujenzi wa msikiti na madrasa kama ambavyo wenzao katika mtaa huo walivyopewa kibali cha kuyatumia maeneo ya umma kujenga makanisa manne.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kamati ya waislamu wa mtaa wa mjimwema ‘B’ Sheikh Haydari Silima Ame, amesema barua yao ya Agost 24/2019 iliyoambatanishwa na muhtasari wa mkutano wa wananchi kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuomba kupewa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa msikiti na madrasa, ilijibiwa Februari 19/2020.

“Tunapenda kuwafahamisha kuwa, maombi yenu yamekubaliwa baada ya kikao cha mipangomiji cha menejimenti kuketi tarehe 10/12/2019”, ilisema sehemu ya barua hiyo yenye Kumb. Na: L30/MMC/6/87.

Hata hivyo barua hiyo ya ofisi ya Mkurugenzi (nakala tunayo) ilibainisha kuwa, wananchi hao wangepaswa kulipia gharama ya ununuzi kiwanja hicho namba 749/B/Tungi, kwa TSH. 30,700,000/-kwa madai kuwa mmiliki wake ni Manispaa ya Morogoro.

Naye mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Bi Mwajuma Tengeni amesema baada ya kupokea barua hiyo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi, walimwandikia tena barua kupitia ofisi ya mtendaji wa mtaa huo kuomba kupunguziwa gharama hizo hasa ikilinganishwa kuwa, wanaohitaji sio Taasisi ya dini, bali ni wakazi waislamu wa mtaa huo ambao wana shida na nyumba ya kufanyia Ibada.

“Sasa basi ningependa kukufahamisha kupitia barua yako kumb Na: L30/MMC/6/87 uliyojibu maombi yao kuwa yamekubaliwa kuwa ni TAASISI, sio TAASISI ni wakazi wa mtaa wa kawaida tu wanaoishi katika mtaa wangu wa mji mwema ‘B’ ambao wanaomba eneo la kawaida la kuabudu (Msikiti)”, ilisema sehemu ya barua ya Machi 30/2020.

Aidha mwenyekiti huyo wa serikali ya mtaa alisema katika mtaa wake kulikuwa na maeneo manne ya wazi ambayo kwa mujibu wa ramani ya Mipangomiji, maeneo hayo yalikuwa yajengwe majengo ya umma (Public Building).

Aliongeza kusema kuwa, maeneo manne tayari yamejengwa makanisa makubwa na waamini wa dini nyingine yanawasaidia kuendelea na ibada zao.

Kwa mujibu wa Bi Tengeni, eneo lililobakia ni hilo ambalo kwa mkutano wa mtaa aliouitisha, wananchi waliridhia eneo hilo pekee lililobaki wapewe wenzao Waislamu ili kuendeleza upendo, umoja na mshikamano wa Kitaifa.

Ilipofika tarehe 27/04/2023 Ofisi ya mtaa wa Mji mwema ‘B’ ilipokea barua kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro yenye Kumb. Na: MMC/LD/14105/14 ikikiri kupokea barua ya Mwenyekiti wa mtaa huo kuomba eneo la wazi lenye matumizi ya umma namba 749/B/Tungi.

“Ofisi itatuma wataalamu wanaohusika na upimaji & ramani siku ya Jumatano ya tarehe 10/05/2023 mchana wa saa saba (7) kamili ili wafanye ukaguzi wa kiwanja unachokikusudia”, ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo tunayo nakala yake.

Hata hivyo Bi Tengeni anasema cha kushangaza wiki iliyopita wanaletewa barua ya April 27/2023 inayodai kuwa, eneo wanaloliomba linamilikiwa na ndugu Jonas Sakara Mugendi wa Dar es Salaam tangu Oktoba 2012.

Licha kwamba barua hiyo imewastua waislamu wa mji mwema ‘B’ lakini pia imewashangaza wananchi wa Kata nzima ya Tungi kusikia eneo la matumizi ya umma la mtaa huo amemilikishwa mtu binafsi!

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bwana Ali Machela ameonesha kusikitishwa kwake na hatua za waislamu wa mtaa huo kujichukulia uwamuzi wa kuanza kujenga bila shauri hilo kufikia mwisho.

“Nasema hivi, siwezi kuwaruhusu kuendelea na ujenzi katika eneo hili mpaka kwanza mubomoe hiki mnachojenga, muondoe tofali na mchanga huu ndipo tukae mezani tuzungumze”, alisema Mkurugenzi huyo ambaye alifika katika eneo hilo na kukuta ujenzi ukiendelea.

Kuhusu mkanganyiko wa eneo hilo kumilikishwa bwana Jonas mkazi wa Dar es Salaam kwa mujibu wa barua ya April 27/2023, Machela alisema hakuna anayemiliki eneo hilo ambalo kwenye ramani ya mipangomiji linaonekana liko wazi.

Kwa upande wake sheikh wa Mkoa wa Morogoro Twaha Swalehe Kilango alipoulizwa Jana kwa njia ya simu na mwandishi wa Habari hizi, alikiri kuwa na taarifa za kina kuhusu sakata hilo na ameahidi kulifuatilia ngazi za juu kwa lengo la kuziomba mamlaka ziwape Waislamu eneo hilo kwakuwa mtaa wa mji mwema 'B' hauna msikiti kwa wakazi wake.

Mpaka tunakwenda mitamboni, Ujenzi wa msikiti katika eneo hilo unaendelea na kesho wameazimia kuswali swala ya Ijumaa.



No comments:

Post a Comment